‘ Mke wangu alikuwa na kifafa na hakuniambia. Nahisi kuhadaiwa ’

Julian  Masese ni jamaa  ambaye amezongwa na mawazo kwani anahisi kusalitiwa na mke wake kwani maajuzi amegundua kwamba, Lisa ana ugonjwa wa kifafa na wakati wote walipokuwa wakichumbiana hakuwahi kumueleza kuhusu hali hiyo yake.

Anasema kugundua kwamba mkewe  ana tatizo hilo sio jambo linalompa hofu bali anashangaa mbona hata jamaa za mke wake alimficha kuhusu hilo na akagundua mwenyewe wakati mke  wake alipoanguka ghafla baada ya kukutwa na shambulizi la kifafa wakiwa nyumbani. Bila kujua kilichokuwa kikifanyika, Julian alikimbia kuwaita majirani ambao mmoja wao alifahamu kwamba shambulizi hilo lilikuwa la kifafa.

Nao hata walishangaa kwamba Julian hakujua kwamba mke wake wa miaka miwili alikuwa na tatizo hilo na hapo ndipo hamaki yake inaanza kuzua makovu. Maswali pia yanaibuka kuhusu vitu ambavyo unafaa kumueleza mwenzako wakati wa uchumba kwa sababu  baadaye, Lisa amejitetea kwamba iwapo Jualian angejua hali yake hapo awali basi angemuacha. Julian anasema hangemtoroka ila angejitayarisha vyema kuweza kukabiliana na hali yoyote ya dharura endapo mkewe angepatwa na shambulizi la kifafa. Zamani  kwa sababu ya ukosefu wa ufahamu kuhusu ugonjwa huo, ilikuwa mwiko sana kwa mwanamme kujihusisha na mwanamke ambaye ana kifafa lakini baada ya mengi kujulikana kuhusu hali hiyo haifai kuwa tatizo katika uhusiano au ndoa.

Ni vyema iwapo mwenzako atajua kwamba una ugonjwa huo ili pawepo mikakati ya kudhibiti  dalili na hatari zinazotokana na shambulizi la kifafa ambalo wakati mwingi huja bila kupangwa. Kwa sasa, kuna dawa   za kudhibiti ugonjwa huo, anti-epileptic drugs (AEDs)  na pia kuna upasuaji ambao unaweza kufanywa ili kuondoa sehemu ya ubongo ambayo humfanya mtu kupatwa na shambulizi la kifafa. Pia watalaam wamegundua njia nyingine ya kuweka kifaa cha eltroniki mwilini kudhibiti mashambulizi ya kifafa Julian anasema endapo Lisa angemueleza kuhusu hali yake,  hatari iliyotokea walipokuwa nyumbani kwao ingeepukika kwa sababu wangekuwa na dawa na njia zote za kudhibiti hali hiyo  .

Katika jamii za kiafrika pia kuna tatizo  la unyanyapaa na aibu  kukubali kwamba jamaa yao ana hali hiyo ya kifafa. Mengi sasa yameanza kujulikana kuhusu tatizo hilo na hakuna anayefaa kuficha hali yake na hasa kwa mpenzi wake. Julian na Lisa wameanza kwenda kumuona mshauri ili kuweza kuzungumzia patashika hiyo nzima kujaribu kuelewa mbona Lisa na jamaa zake walimficha Julian kuhusu hali yake kwani hatua hiyo ina hatari ya kuvuruga ndoa yao changa.