Kunani? Wakuu wa maabara Tanzania wasimamishwa kazi, uchunguzi wafunguliwa dhidi yao

AFRIKA
AFRIKA
Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ya Tanzania Dkt Nyambura Moremi na Meneja wa Udhibiti wa Ubora wa maabara hiyo Jacob Lusekelo wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Hatua hii inakuja siku moja baada ya Rais John Magufuli kutilia shaka utendaji wa upimaji wa virusi vya corona   (COVID-19) katika maabara hiyo. Akihutubia katika shughuli ya uapisho wa waziri mpya wa Katiba na Sheria, Rais Magufuli alifichua kwamba hivi karibuni zilitumwa sampuli zisizo za binadamu katika maabara hiyo kwa siri na kurudisha baadhi ya majibu yakionyesha uwepo wa maradhi ya COVID-19 kwa wanyama, ndege na matunda.

"Sampuli ya oili kwa mfano iliyotoka kwa gari, tuliipa jina la Jabir Hamza mwenye miaka 30, ile ilileta negative. Tulipopeleka sampo ya fenesi, ambayo tuliipa jina la Sarah Samweli, miaka 45, matokeo yake yalikuwa unconclusive. Tulipopeleka sampo ya papai tukaipa jina Elizabeth Anne miaka 26 papai lile lilikuwa positive," alisema Magufuli.

Magufuli aliongeza pia kwamba sampuli kutoka kwa ndege aina ya kware na mbuzi zilikutwa na maambukizi ya COVID-19 huku sampuli ya sungura haikuwa na matokeo kamilifu.Taarifa kutoka Wizara ya Afya inasema, waziri wa afya ameunda tume ya watu 10 kuchunguza mwenendo wa maabara hiyo ya taifa na kwamba itatakiwa kuwasilisha taarifa yao ifikapo tarehe 13 Mei, 2020. Hata hivyo taarifa imesema upimaji wa sampuli katika maabara hiyo utaendelea kama kawaida. Tanzania imekuwa ikikosolewa juu ya namna inavyopambana na COVID-19 kwamba haijachukua hatua kali vya kutosha huku utendaji wa serikai ukishutumiwa kugubikwa na usiri.

Hata hivyo, serikali imekana shutuma hizi na kusema inazingatia kikamilifu miongozo inayotolewa na shirika la afya ulimwenguni (WHO). Kwa mujibu wa takwimu za mwisho zilizotolewa na Wizara ya Afya mnamo tarehe 29 April, Tanzania ina jumla ya idadi ya wagonjwa 480, hii ikiwa ni pamoja na idadi ya vifo 16, huku idadi ya waliopona ikiwa ni wagonjwa 167.