Likoni: Gari lililowabeba wahadhiriwa huenda kuwa limepatikana - Oguna

MV Likoni
MV Likoni
Gari ambalo lilikuwa limewabeba mama na mwanawe ambao walikufa maji katika bahari ya hindi laweza kuwa limepatikana, msemaji wa serikali Cyrus Oguna ametangaza.

Hata hivyo alisema kuwa serikali bado haijathibitisha ingawa nambari ya usajili ya gari hilo inafanana na ile iliyokuwa imewabeba Mariam Kighenda, 35, na Amanda Mutheu, 4.

Msemaji huyo wa serikali alionekana kumpasha mpiga mbizi kutoka Uswidi ambaye alikuwa amesema kuwa anaweza okoa miili hiyo na masaa mawili pekee.

"Kuna watu waliokuja wakijifanya kuwa wanaweza okoa miili, lakini walishindwa na wakaenda," Alisema.

Mpiga mbizi huyo, Volker Bassen baadaye aligeuza maneno yake na kusema kuwa alikuwa amedharau hali halisi.

Pia alisifu kikosi cha wanamaji kwa juhudi zao, akisema wanafanya kazi njema.

Oguna alisema, "Tumefanya kila juhudi kutafuta miili hiyo pamoja na gari."

Jumanne jioni, kikosi cha wanamaji kilitangaza kuwa kilikuwa kimeona kifaa chini ya bahari hindi baada ya kutumia teknolojia mpya katika juhudi za kuitafuta miili hiyo.

Mariam na Amanda walifariki September 29, baada ya gari lao kuteleza kutoka ferry ijulikanayo kama, MV Harambee na kuingia kwenye bahari hindi.