Mama ateketezwa kwa madai ya ushirikina Bungoma

Familia moja kutoka kijiji cha Burangasi eneo bunge la Bumula huko Bungoma inalilia haki baada ya mama Evelyn Nasimiyu kuvamiwa na kundi la vijana na kuteketezwa kwa madai ya ushirikina.

Kutokana na majeraha aliyopata Nasimiyu alilazwa katika hospitali ya rufaa ya Bungoma kwa zaidi ya miezi miwili kabla ya kufariki, huku familia ikishindwa kulipia gharama ya matibabu na hivyo mwili wake kuzuiliwa katika hifadhi ya wafu ya hospitali hiyo kwa mwezi mmoja sasa.

Familia hio ambayo ni chochole, sasa inaitaka serikali ya kaunti ya Bungoma kuingilia kati na kuwasaidia kuondoa gharama, baada ya gharama ya hospitali na mochari kuishinda familia kulipia kama anavyosimulia Wycliffe Khaemba mumewe marehemu.

Chifu wa eneo hilo Julius Nyongesa anaitaka serikali ya kaunti kuondoa gharama hiyo ili familia hiyo iweze kumzika mpendwa wao kwa njia nzuri akiahidi kuwa usalama upo shwari.

Kisa hiki ni cha pili kutokea katika eneo bunge hili huku kisa sawia kikitokea katika eneo la khasoko baada ya mtu mmoja kuteketezwa hadi kufa kwa madai ya ushirikina.

-Brian Ojamaa