Mama Margaret Kenyatta aanzisha mbio za wanaume 100 kwenye Msitu wa Karura

kenyatta
kenyatta

 Mama wa Taifa Margaret Kenyatta hii leo alizindua harakati za mwaka huu za Mbio za Beyond Zero Half Marathon kwa kuanzisha mbio za wanaume 100 katika Msitu wa Karura.

Mbio hizo za wanaume pekee, zenye kauli mbiu ‘I will Run For Her’, zinatangulia mbio za mwaka huu za Beyond Zero Half Marathon ambazo zimepangwa kufanyika tarehe 8 mwezi Machi.

Shughuli hiyo iliandaliwa kuwiana na Siku ya Wapendanao na wanaume walikuwa wakikimbia kuunga mkono na kuboresha mchango wao kuhusiana na maswala ya afya ya akina mama na watoto ambayo yanaathiri mama zao, wake, dada, na mtoto wa kike.

Hii ni pamoja na upasuaji na kuwakubali wanawake walio na matatizo ya nasuri, kupigia debe kukomeshwa kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi na ugonjwa wa kaswende kutoka kwa mama hadi kwa mtoto mchanga kufikia mwaka wa 2021, kuendeleza lishe bora kwa watoto wote na kuhimiza kuhusishwa kikamilifu katika masuala ya kijamii kwa watoto walio na ulemavu ili wapate huduma sawa na wengine za afya na elimu kati ya zingine.

Kinyume na makala ya awali ya mbio za marathon, mwaka huu washiriki watachagua nyanja ambayo wanaunga mkono katika mfumo pana wa afya ya mama na mtoto. Nyanja hizo ni pamoja na kumaliza vifo vya akina mama, kumaliza vifo vya watoto, mtindo bora wa maisha kwa wakongwe, kukabili maambukizi mapya ya virusi vya HIV pamoja na kumaliza ndoa za mapema.

Nyanja zingine ni kukabili ukeketaji wa wanawake (FGM), uchunguzi wa mapema dhidi ya saratani, kuhusisha watu walio na ulemavu pamoja na lishe bora kwa watoto wote.

Mama wa Taifa akiwa ameandamana na Mawaziri Amina Mohamed, Sicily Kariuki na Margaret Kobia pamoja na Mshauri Mkuu katika Ofisi ya Mama wa Taifa Constance Gakonyo, Afisa Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Kukabiliana na Maradhi ya Ukimwi Dkt Nduku Kilonzo na wanachama wa uhazili wa shirika la Beyond Zero alijiunga kwenye shughuli ya kupasha misuli moto kabla ya kuanza kwa mbio hizo za wanaume pekee.

Miongoni mwa walioshiriki mbio za leo katika Msitu wa Karura ni Waziri wa Mazingira na Misitu Keriako Tobiko na Mkuu wa Sheria Paul Kihara Kariuki.

Vilevile, miongoni mwa kundi hilo la wanaume 100 walioshiriki mbio hizo za asubuhi ni Afisa Mkuu wa kampuni ya Bima ya Jubilee Dkt Julius Kipng’etich, Rais wa Chama cha Riadha nchini Luteni Jenerali Mstaafu Jackson Tuwei pamoja na mwandishi wa habari za michezo wa runinga ya Citizen Mike Okinyi na mwenzake wa Capital FM Alex Isaboke kati ya wengine.

Mama wa Taifa ambaye aliwapokea washiriki mwishoni mwa mbio hizo baadaye alipanda mti kwenye Msitu wa Karura kuashiria umuhimu wa shughuli hiyo na kujitolea kwake katika uhifadhi wa mazingira.

Fedha zitakazokusanywa kutokana na mbio za mwaka huu za Beyond Zero Half Marathon zitatumika kwa mandalizi ya harakati za Medical Safaris, ambao ni mpango mpana unaotekelezwa kwa ushirikiano na serikali za kaunti na zaidi ya wahudumu wengine 15 wa kutoa huduma za afya.

Mpango wa Beyond Zero hutoa huduma za afya bila malipo kwenye harakati za medical safaris wa kupeleka huduma mashinani. Kufikia sasa, shirika la Beyond Zero limeandaa kambi tano zilizofana katika kaunti ya Nairobi, Nyandarua, West Pokot, Kisumu na Narok.

-PSCU