Mama mkwe alinishauri nimtafute mke wangu kupitia patanisho - Kiragu

Bwana Kiragu alituma ujumbe akiomba apatanishwe na mkwe bi Doreen akidai kuwa wawili hao walitengana miaka miwili iliyopita.

"Nilikuwa na tabia ya kubugia pombe na alikuwa ananionya kuwa ataniwacha, nilidhania ni mchezo na siku moja nikapata ameondoka. Nimekuwa nikimpigia simu na kila ninapoenda kwao kumshawishi arudi huwa hakubali." Alieleza Kiragu.

Kinachomsumbua Kiragu ni kuwa ana umri wa miaka 40 na hajui ataanzaje ki maisha kwani hata akaja amua kuoa tena itambidi aoe mwanamke mwenye watoto tayari.

Anasisitiza kuwa tangia atengwe na mkewe ameacha pombe kwani ameteseka sana.

Wawili hao wamekuwa kwa ndoa ya miaka kumi na wamejaliwa mtoto mmoja.

Kiragu alidai kuwa wazazi wa mkewe hawana shida naye na wangependa warudiane na isitoshe, mama mkwe ndiye aliyempa mawaidha atafute usaidizi, Radio Jambo kupitia kitengo cha Patanisho.

"Doreen anapenda kuskiza Patanisho za wenyewe na ndio maana mama mkwe aliniambia nitafute usaidizi kutoka kwenu." Aliongeza Kiragu.

Hata hivyo Doreen hakujibu simu zetu na ilibidi tusitishe shughuli za kuwapatanisha wawili hao.