Mbunge mteule wa chama cha Jubilee Maina Kamanda ameashiria kwamba viongozi wa eneo la kati huenda wakamwunga mkono waziri wa usalama wa ndani kuwa waziri mkuu chini ya mapendekezo yaliyotolewa na jopokazi la BBI .Kamanda amemlimbikizia sifa Matiangi akisema waziri huyo ndiye anayeilinda serikali ya rais Uhuru Kenyatta . Mbunge huyo aliyasema hayo akiwa Kisii wakati wa mkutano wa kwanza wa ushauriano kuhusu BBI uliowaleta pamoja viongozi kadhaa kutoka sehemu mbali mbali za taifa wakiongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga .Kamanda aliwahimiza wakaazi wa Kisii Kumlinda ‘mwanao’ Matiang’I ili wakati mwafaka utakapowadia eneo la mlima Kenya Litamwunga mkono awe waziri mkuu .
" Hata kazi inayofanywa na mawaziri kutoka kati haiwezi kulinganishwa na kazi anayofanya Matiang'i’ Kamanda alisema huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo . Wakati wa mkutano huo , Raila alisema jitihada za BBI ndio njia pekee ya kuwafikisha wakenya ‘Canaan’.
Raila amesema taifa litaunganishwa na BBI baada ya mwafaka wa ushirikiano kati yake na rais Uhuru Kenyatta machi mwaka wa 2018 .Raila amesema kutakuwa na mikutano zaidi ya ushauriano kuhusu BBI katika sehemu mbali mbali za taifa kuwaelimisha wakenya kuhusu yaliyomo katika ripoti hiyo.Matiang'i aliwasifu Raila na Uhuru kwa umoja unaoshuhudiwa nchini kwa sasa na kuwahimiza Viongozi wa Nyanza kusalia na umoja ." Hii ndio mara ya kwanza tunaketi pamoja kama viongozi wa Nyanza ili kujadili kuhusu msimamo mmoja tunaoutaka’ amesema Matiang’I . Matiang’I amewashauri waakilishi wa kaunti kuandaa hafla za kuijadili ripoti ya BBI na wakaazi wa wadi zao .