Matokeo ya mtihani wa KCPE yako tayari kutolewa, atangaza Rais Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta leo ametangaza kwamba kusahihishwa kwa mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi, KCPE, kumekamilika na matokeo yako tayari kutolewa.

Wakati huo huo, Rais alisema kwamba mtihani wa mwaka huu wa KCPE haukukumbwa na visa vya udanganyifu na kasoro  zozote zile.

“Kulikuwa na visa vichache  sana vya udanganyifu au ukiukaji sheria wakati wa mtihani wa mwaka huu na nawashukuru wazazi, walimu na watahiniwa. Tungependa kuwapongeza wale wote waliochangia ufanisi kwenye mtihani huo,” kasema Rais.

Rais Kenyatta alisema haya katika kijiji cha Gachororo, eneo wakilishi bunge la Juja ambako alihudhuria ibada ya Jumapili na kuongoza shughuli ya kuchangisha pesa za kusaidia ujenzi wa kanisa jipya la PCEA.

Rais alisistiza ahadi yake ya hivi majuzi kwamba hakuna mtahiniwa aliyefanya mtihani wa KCPE atakosa nafasi ya kujiunga na shule ya upili.

Alitoa wito kwa wazazi wa watahiniwa wa KCPE kuhakikisha watoto wao wanajiunga na shule za upili kwa sababu nafasi zao tayari zipo na Serikali itagharamia elimu yao.

Vile vile, Rais  alisistiza matamshi yake ya hivi majuzi kwamba kanisa linastahili kutekeleza wajibu mkubwa kuimarisha maadili ya taifa.

Alisema Kenya imekuwa ikitambuliwa kuwa nchi ya imani kuu lakini hivi karibuni imeonekana kupoteza mwelekeo wake wa maadili.

“Lazima turejeshe mfumo wa maadili ya taifa letu kupitia ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa,”kasema Rais.

Vile vile, Rais Kenyatta alitoa wito kwa wabunge kupitisha Mswaada kuhusu usawa wa kijinsia ili kutimiza mahitaji ya katiba.

“Hebu tuwajibike kwa mjibu wa katiba na kupitisha sheria kuhusu usawa wa kijinsia,” kasema Rais.

Viongozi wengine waliohutubu katika kanisa hilo ni kiongozi wa wengi katika Bunge la Seneti Kipchumba Murkomen, Gavana wa Kaunti ya Kiambu Ferdinand Waititu na Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi.

Rais Kenyatta alisimama mjini Juja kuitikia salamu za wananchi kabla ya kuwahutubia kwa muda mfupi.