Mbunge wa Kibra Ken Okoth akimbizwa hospitalini

Mbunge wa Kibra Ken Okoth alikimbizwa hospitalini katika hospitali ya Nairobi, chumba cha wagonjwa walio katika hali mahututi jana usiku.

Hii ni baada yake kutokea mbele ya wananchi wiki kadhaa baada ya kuwa Ufaransa kwa mda wa miezi mitano ambako alikuwa anapokea matibabu ya ugonjwa wa saratani.

Alikuwa amehudhuria tamasha za Kibra Music Fest katika shule ya upili ya wasichana ya Moi, Nairobi.

Mwezi Mechi mwaka huu, Okoth aliambia wakenya kuwa anaugua ugonjwa wa Saratani ya tumbo na kuwa ana matumaini ataishi.

Okoth, 41, anahudumia wananchi wake kwa mara ya pili bungeni.

Alionesha ujasiri kuwa atashinda vita hiyo dhidi ya hayawani huyo katika mtandao wake wa Twitter huku akimjibu Benjie Wambui, ambaye alikuwa anamjulia hali.

"How are you Mheshimiwa? Nakuombea sana leo,” Wambui alikuwa ameandika.

Okoth alijibu, “Napambana na hali yangu na tutashinda.”

Tunamtakia mheshimiwa Okoth uponyaji.

Mapema mwezi huu, wakenya kutoka tabaka mbali mbali katika mtandao wa kijamii wa Twitter walionesha umoja wao na kuzidi kumuombea Okoth.

Hii ni baada ya picha yake Ken Okoth ambaye kuchapishwa mtandaoni na balozi wa Kenya nchini Ufransa, Judi Wakhungu baada ya mkutano kati ya wawili hao.