Mhudumu wa bodaboda auawa baada ya kuiba kuku wanne

Mhudumu wa bodaboda ambaye alikuwa na miaka 26 aliuawa jana jioni na umati uliojaa hasira katika kijiji cha Kandeto eneo la Munyeki Ol kalaou.

Eric Kihonge barubaru anayetoka mtaa wa Gikumbo eneo la Ol kalou karibu kilomita 10 kutoka mtaa wa Kandeto aliuawa baada ya kukamatwa na kuku wanne ambao alikuwa ameweka ndani ya gunia.

Dominic Kipkoech Cheriot ambaye anaaminika kusaidiana na Eric kutekeleza uhalifu huo wa kuiba aliponea kifo baada ya kutoroka na kujisalimisha katika ofisi ya naibu wa kamishna wa kaunti huko Ol kalou ambapo aliokolewa na polisi na baadaye kufikishwa katika kituo cha polisi na kufungwa.

Polisi walikuwa na wakati mgumu kutuliza umati huo ambao ulikuwa unataka kuchukua sheria mikononi mwao.

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Nyandarua Leonard Kimaiyu, alieleza asubuhi ya leo kwamba wakazi kupitia nambari ya simu ya polisi waliripoti kuwa Kihonge alipatikana na kuku ambae alikuwa amethibitishwa na wakazi hao kuwa amibiwa na pindi alipogunduliwa alijaribu kutoroka lakini alishikwa na wakazi hao wenye hamaki akapigwa na kuuawa.

Polisi walifika katika eneo hilo na kumkimbiza hospitalini lakini alikuwa amekata kamba. Waendeshaji wa bodaboda walisema kuwa Kihonge saa zingine angewacha piki piki yake kwenye klabu ili aende kutekeleza visa vya uhalifu.
Afisa wa polisi alisema kuwa kuku hao wanne bado wako katika kituo cha polisi na wamiliki bado hawajajulikana kwani hakuna yeyote aliyejitokeza na kudai kuku hao.