Divock Origi atia saini mkataba wa mda mrefu na Liverpool

Divock Origi ametia saini mkataba wa muda mrefu na Liverpool kufuatia msururu wa kushinda mechi msimu uliopita.

Mshambulizi huo wa Ubelgiji ambaye alikua amesalia na mwaka mmoja kwenye kandarasi yake alifunga mabao mawili wakati Liverpool walipowanyuka Barcelona mabao 4-0 katika nusu fainali ya Champions League.

Origi pia alifunga balo la pili katika fainali yao ya Champions League dhidi ya Tottenham, na walipowanyuka Newcastle na Everton katika ligi ya Premier.

Huko Uhispania, Barcelona inataka kumsajili beki wa Manchester United na raia wa Uswidi Victor Lindelof mwenye umri wa miaka 24, huku ikiwa beki wa Ajax Matthijs de Ligt anatarajiwa kujiunga na Juventus.

Kwingineko Real Madrid watalazimika kulipa dau litakalovunja rekodi ya pauni milioni 162 kumsajili kiungo wa kati wa Ufaransa Paul Pogba mwenye umri wa miaka 26, kutoka Manchester United.

Huko Uingereza, duru zilizo karibu na Wilfried Zaha zinaashiria kuwa kuna tashwisi ya iwapo Arsenal wataweza kumsajili kutoka Crystal Palace.

The Gunners wanamtaka raia huyo wa Ivory Coast na walikua wametoa ofa ya pauni milioni 40 mapema mwezi huu. Hata hivyo Palace walikataa ofa hiyo na wanaaminika kumwekea Zaha thamani ya pauni miliono 80.

Tukirejea Afrika, William Troost-Ekong alifunga bao la dakika za lala salama na kuisadiai Nigeria kufuzu kwa nusu fainali ya michuano ya AFCON kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Afrika Kusini.

Samuel Chukwueze alianza kufunga kabla ya Bongani Zungu kusawazisha. Nigeria watakabana na Ivory Coast au Algeria jumapili. Kwingineko Senegal ilifuzu kupitia kwa bao la kiungo wa kati wa Everton Idrissa Gueye walipowanyuka Benin.

Senegali watakabana na Madagascar au Tunisia katika nusu fainali jumapili jijini Cairo.