Omanyala azungumza baada ya kutwaa dhahabu kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola

Omanyala alimaliza wa kwanza baada ya kukimbia kwa sekunde 10.02.

Muhtasari

•Omanyala aliishindia Kenya dhahabu ya kwanza kabisa katika mbio za mita 100 kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola.

•Omanyala amesherehekea ushindi wake na kuwashukuru wote waliounga mkono azma yake ya kutwaa ubingwa.

ashinda dhahabu kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola jijini Birmingham, Uingereza mnamo Agosti 4, 2022.
Ferdinand Omayala ashinda dhahabu kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola jijini Birmingham, Uingereza mnamo Agosti 4, 2022.
Image: HISANI

Ferdinand Omanyala sasa sio tu bingwa wa Kenya na Afrika bali pia ni bingwa wa Jumuiya ya Madola mwaka wa 2022.

Jumatano usiku mwanaspoti huyo mahiri aliishindia Kenya dhahabu ya kwanza kabisa katika mbio za mita 100 kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola.

Omanyala alimaliza wa kwanza katika mashindano yanayoendelea jijini Birmingham, Uingereza baada ya kukimbia kwa sekunde 10.02.

Akani Simbine wa Afrika Kusini alimaliza nyuma ya Omanyala kwa sekunde 10.13 huku Yupun Abeykoon wa Sri Lanka akichukua nafasi ya tatu baada ya kukimbia kwa sekunde 10.14.

Pengo kubwa (sekunde 0.11) kati ya bingwa huyo anayeshikilia rekodi ya Afrika katika mbio za mita 100  na aliyeibuka wa pili linaonyesha wazi kuwa aling'aa zaidi mno  ya wapinzani wake.

Omanyala amesherehekea ushindi wake na kuwashukuru wote waliounga mkono azma yake ya kutwaa ubingwa.

Isaya 55.5 , Kwa utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Asanteni sana kwa uungwaji mkono na motisha," Omanyala alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Aliongeza "BINGWA WA AFRIKA sasa ndiye BINGWA WA JUMUIYA YA MADOLA!"

Wakenya wengi wameendelea kumpongeza bingwa huyo wa mbio za mita 100  kupitia mitandao ya kijamii.

Ushindi huu wake unajiri wiki chache tu baada ya kuandikisha matokeo ya kukatosha tamaa huko Oregon, Marekani.

Mwezi jana Omanyala alibanduliwa nje ya mashindano ya dunia katika hatua ya nusu fainali baada ya kumaliza wa tano katika kundi alilowekwa.

Kucheleweshwa kwa safari yake kuenda Marekani kulinyooshewa kidole cha lawama kufuatia matokeo hayo kwani ni wazi kuwa hakupata muda tosha wa kujiandaa.

Hata hivyo mwanaspoti huyo sasa ana sababu za kutabasamu kwani hatimaye ameweza kung'aa katika jukwa la kimataifa

Hongera bingwa wetu Ferdinand Omanyala!