Mandonga ‘Mtu Kazi’ apoteza pambano lingine kwa kupigwa TKO ya kidevu katika raundi ya 6

Baada ya kuhimili ngumi kwa raundi kadhaa, Mandonga alishindwa kustahimili uzito wa ngumi ya Maugo iliyolenga na kumpata barabara kwenye kidevu na kumdondosha sakafuni katika raundi ya 6.

Muhtasari

• Pambano hilo lilipewa jina Vitasa Face Off na Mandonga aliingia ulingoni kuzichapa dhidi ya bondia mwingine kwa jina Mada Maugo.

• Baada ya pambano, Maugo alisema amekuwa akipatiwa mafunzo na mke wake na alimpa ujanja wa kutoyumbishwa na papara za Mandonga wakati wa kupambana naye.

Karim Mandonga
Karim Mandonga
Image: Instagram

Bondia wa Tanzania mwenye vishasha na vimbwanga vingi, Karim Mandonga maarufu kama ‘Mtu Kazi’ kwa mara nyingine ameonyeshwa kivumbi katika ulingo baada ya kuondolewa kwa Technical Knock Out – TKO – katika raundi ya 6 ya pambano la ngumi lililoandaliwa mjini Morogoro nchini humo.

Pambano hilo lilipewa jina Vitasa Face Off na Mandonga aliingia ulingoni kuzichapa dhidi ya bondia mwingine kwa jina Mada Maugo.

Baada ya kuhimili ngumi kwa raundi kadhaa, Mandonga alishindwa kustahimili uzito wa ngumi ya Maugo iliyolenga na kumpata barabara kwenye kidevu na kumdondosha sakafuni katika raundi ya 6 na kumfanya mwamuzi Pendo Njau kuingilia kati na kumaliza pambano kwa kumtangaza Mada kuwa mshindi.

Baada ya pambano, Maugo alisema amekuwa akipatiwa mafunzo na mke wake na alimpa ujanja wa kutoyumbishwa na papara za Mandonga wakati wa kupambana naye.

“Mwalimu wangu ambaye ni mke wangu aliniambia niwe na utulivu ulingoni, hilo nimelitimiza, nikikutana na Mandonga popote pale bado nitampiga tena.”

Upande wa Mandonga alisema “Maugo hawezi kunisumbua, ni mchezo tu, uwezo wa kunipiga hana.”

Licha ya kuwa na maneno mengi ya vitisho kwa washindani wake, Mandonga amekuwa akichezea kipigo mikononi mwa kila bondia ambaye amekuwa akikutana naye, haswa katika kipindi cha mwaka jana na mwaka huu.

Hata hivyo, Mandonga sasa anatarajia kuziamsha popo zake kwenye mwili wa msanii Harmonize, endapo msani huyo atakubali kupigana naye baada ya kudai kwamba anataka kuzichapa dhidi ya bondia mwingine kwa jina, Mwakinyo.