FIFA kuifurusha Kenya ikiwa Mwendwa atatimuliwa na serikali

Muhtasari

• Katika barua kwa katibu mkuu wa shirikisho la FKF Barry Otieno siku ya Alhamisi, FIFA ilisema kwamba kulingana na sheria za FIFA waziri hana mamlaka kufurusha maafisa wa shirikisho la soka.

debts
debts

Shirikisho la soka duniani FIFA limetishia kuifurusha Kenya kutoka soka ya kimataifa ikiwa waziri wa michezo Amina Mohamed hatabatilisha uamuzi wa kumfurusha rais wa FKF Nick Mwendwa.

Katika barua kwa katibu mkuu wa shirikisho la FKF Barry Otieno siku ya Alhamisi, FIFA ilisema kwamba kulingana na sheria zake waziri hana mamlaka kufurusha maafisa wa shirikisho la soka.

“Kwa hakika, mashirikisho yote wanachama wa FIFA, ikiwa ni pamoja na FKF, yanahitajika kisheria kusimamia mambo yao kwa uhuru na bila ushawishi usiofaa wa wahusika wengine,” barua ya FIFA ilieleza.

 Kulingana na FIFA marufuku dhidi ya Kenya itaathiri shughuli zote za kandanda  na sio tu watu binafsi ambao huenda walihusika kwa njia moja au nyingine pekee.

Barua hiyo iliyotiwa saini na afisa wa FIFA Kenny Jean-Marie ilitoa wito kwa waziri kuzingatia kwa makini sheria za FIFA na uhuru wa shirikisho la FKF ili kuzuia Kenya isipigwe marufuku.

“Kwa hivyo, tunakuomba umfahamishe waziri kwamba ikiwa uamuzi wake wa kuteua Kamati ya Uangalizi ya FKF na sekretarieti inayohusika utazingatiwa, hatutakuwa na budi ila kuwasilisha suala hili kwa Ofisi ya Baraza la FIFA kwa kwa uamuzi wake,” barua hiyo ilieleza. 

Hata hivyo shirikisho la FIFA lilisema kwamba liko tayari kuandaa mkutano wa pamoja baina ya shirikisho la FKF na waziri wa michezo kujadili mzozo baina ya pande hizo mbili na kushughulikia madai yaliyoibuka.

“...tungependa kusisitiza kuhusu nia yetu kufanya mkutano baina ya FKF na Wizara ya Michezo haraka iwezekanavyo ili kushughulikia wasiwasi wowote ambao pande zote mbili zinaweza kuwa nao na, kwa pamoja, kuamua njia ya kusonga mbele kwa ajili ya soka ya Kenya”. 

Waziri wa Michezo Amina Mohamed alifurusha usimamizi wa shirikisho la soka nchini chini ya rais wa FKF Nick Mwenda kwa kipindi cha miezi sita kutokana na madai ya ubadhirifu wa fedha na kuteua kamati ya muda kusimamia shughuli za soka.