Benjamin Mendy: Mchezaji wa Manchester City ashtakiwa kwa makosa mengine mawili ya ubakaji

Muhtasari

•Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 27, ambaye bado yuko kizuizini, sasa anakabiliwa na makosa sita ya ubakaji na moja la unyanyasaji wa kingono.

Benjamin Mendy
Benjamin Mendy
Image: PA MEDIA

Beki wa Manchester City Benjamin Mendy ameshtakiwa kwa makosa mengine mawili ya ubakaji.

Bw Mendy, wa Prestbury, ameitwa kufika katika Mahakama ya Stockport Magistrate' siku ya Jumatano.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 27, ambaye bado yuko kizuizini, sasa anakabiliwa na makosa sita ya ubakaji na moja la unyanyasaji wa kingono.

Mashtaka hayo yanawahusu walalamikaji wanne wenye umri wa zaidi ya miaka 16 na yanadaiwa kutendeka kati ya Oktoba 2020 na Agosti 2021.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa amewachezea mabingwa wa Ligi Kuu ya England msimu uliopita Manchester City tangu 2017, alipojiunga kutoka Monaco kwa kitita cha pauni milioni 52.

Alisimamishwa na klabu hiyo baada ya kufunguliwa mashtaka na polisi, huku uchunguzi ukiendelea.

Louis Saha Matturie pia hapo awali alishtakiwa kwa makosa manne ya ubakaji kuhusiana na madai ya mashambulizi kati ya Machi 2021 na Agosti 2021.

Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 40 kutoka Eccles pia ameshtakiwa kwa makosa mawili ya ziada ya ubakaji na moja la unyanyasaji wa kijinsia na kutakiwa kufika katika mahakama hiyo.

Wawili hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani tarehe 24 Januari mwaka 2022.