Mmiliki wa Chelsea anaripotiwa kupigwa marufuku kuishi Uingereza

Muhtasari

• Mmiliki wa klabu cha soka cha Chelsea, bilionea Mrusi Roman Abrahamovic anaripotiwa kupigwa marufuku kuishi nchini Uingereza.

• Marufuku hii inatajwa kuwa ni sababu za bilionea huyo kuwa mmoja kati ya wawezeshaji wakubwa wa sera za rais wa Urusi, Vladmir Putin.

Mmiliki wa klabu ya Chelsea, Roman Abrahamovic
Image: Chelsea Fottball Club (Facebook)

Mmiliki wa klabu cha soka cha Chelsea, bilionea Mrusi Roman Abrahamovic anaripotiwa kupigwa marufuku kuishi nchini Uingereza kwa kile mamlaka za uhamiaji nchini humo zilisema bilionea huyo ni mmoja kati ya watu ambao wanashabikia hatua za rais wa Urusi, Vladmir Putin kuishambulia Ukraine.

Fununu hizi za kupigwa marufuku zinakuja siku chache tu baada ya Wabunge wa Uingereza kusema kwamba Abrahamovic yupo miongoni mwa orodha iliyotolewa na kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexie Navalny kuwa ni mmoja kati ya wakereketwa wakubwa wa sera za rais Putin na ni mwezeshaji mkubwa wa sera hizo.

Abrahamovic anasemekana kupinga vikali madai hayo kwa kusema kwamba hayupo hata karibu na vitendo hivyo vya Putin ambavyo vinaweza pelekea mataifa mbalimbali ya Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo kadha wa kadha kutokana na kukaidi onyo na ushauri wa kutoishambulia Ukraine.

Ikumbukwe hii haitakuwa mara ya kwanza kwa bilionea huyo kupigwa marufuku kuingia Uingereza kwani mwaka 2018 alipigwa marufuku kuingia huko kama Mrusi ila akakubaliwa kuingia tena na visa yake ya Israel ambapo alikaa kwa muda mchache. Lakini safari hii taarifa kutoka shirika la The Sun zinasema kwamba jaribio lolote la bilionea huyo kujaribu kuweka ombi la kutaka visa ya Uingereza litakataliwa kabisa kwa kuhusishwa na sera za rais Putin.

Abrahamovic alitua nchini Uingereza mwaka 2003 na kununua klabu ya Chelsea ambapo kwa muda sasa amekiboresha klabu hicho mpaka kuwa timu kubwa ambayo chini ya umiliki wake imeshinda mataji mbalimbali ndani na nje ya Uingereza.