(+video) B.Fernandes akataa kumsalimia Ronaldo baada ya kuisema vibaya Man-U

Katika video hiyo, Fernandes anaingia kwenye chumba na kumkuta Ronaldo ambapo anadinda kumnyooshea mkono kwa ajili ya salamu.

Muhtasari

• Katika video hiyo, Bruno anaondoka eneo hilo huku akimwaacha Ronaldo akiwa bado amenyoosha mkono pasi na kuamini kile alichotendewa na Mreno mwenzake.

Baada ya staa wa Ureno Christiano Ronaldo kuachia kashfa kali dhidi ya timu yake ya Manchester United, mchezaji huyo sasa ana kibarua cha kuiongoza timu yake ya taifa ya Ureno katika kipute cha kombe la dunia.

Ronaldo na wenzake kwa mara ya kwanza walikutana katika kambi ya mazoezi kwa ajili ya maandalizi kuelekea Qatar kushiriki kombe la dunia.

Kilichowashangaza wengi ni baada ya kukutana na mchezaji mwenza Bruno Fernandes ambaye pia wanacheza timu moja ya Man U, na mchezaji huyo kulingana na video ambayo imesambazwa mitandaoni alionekana kutofurahia kumsalimia kabisa Ronaldo.

Mahojiano ya Cristiano Ronaldo yanaonekana kuwakera watu wengi wanaohusishwa na Manchester United tangu alipoamwaga mtama Jumapili, 13 Novemba.

Katika video hiyo, Bruno anaingia na kumkuta Ronaldo amesimama kando ya rafu ya kuwekea bidhaa za spoti na kumpita bila kumsalimia.

Baadae Ronaldo anamgusa mgongo na Fernandes anageuka ka kumgusisha mkono kwa dharau kabla ya kuondoka eneo hilo.

Ronaldo anaonekana amebaki kinywa wazi huku mkono wake ukiwa umebaki umenyooshwa asiweze kuamini kitendo kile kutoka kwa Mreno mwenzake aliyeonekana kukerwa kweli na matamshi ya Ronaldo dhidi ya timu ya Man U.

Mahojiano ya Ronaldo na mtangazaji maarufu na mwenye utata Piers Morgan yalifanyika Jumapili, na maelezo hayo yaliwaacha mashabiki wengi wa Man United wakiwa na hasira, hasa shutuma zake kwa kocha Erik ten Hag.

Mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or pia alimchamba moja kwa moja mchezaji mwenzake wa zamani Wayne Rooney, meneja wa muda wa zamani wa United Ralf Rangnick na klabu yenyewe. Mahojiano hayo yalikuja baada ya United kushinda 2-1 dhidi ya Fulham.