Kombe la dunia kupeperushwa moja kwa moja mtandaoni Twitter - Elon Musk

Jumapili Novemba 20, Wenyeji Qatar watafungua uwanja dhidi ya Ecuador.

Muhtasari

• Mechi ya kwanza ya Kombe la Dunia Jumapili! Tazama kwenye Twitter kwa matangazo bora - Musk alisema.

Image: Hisani

Mkurugenzi mkuu mpya wa mtandao wa Twitter, Elon Musk ametangaza habari mpya kwa wapenzi wa soka kuhusu kipute kikubwa zaidi cha kandanda duniani kitakachong’oa nanga Jumapili nchini Qatar.

Musk aliweka wazi kwamba mechi ya kwanza kabisa ya kufungua mashindano ya kombe la dunia baina ya Qatar na Ecuador itatangazwa na kuoneshwa moja kwa moja kwenye mtandao wa Twitter.

“Mechi ya kwanza ya Kombe la Dunia Jumapili! Tazama kwenye Twitter kwa matangazo bora na maoni ya wakati halisi,” Elon Musk alisema.

Tangu kufanikiwa kuchukua mtandao huo kwa dau la dola bilioni 44 za Kimarekani, amekuwa akitangaza mabadiliko na mageuzi kadhaa kwenye mtandao huo, ikiwemo kuwafuta mamia ya wafanyikazi wa kutegemewa zaidi.

Awali tajiri huyo wa Space X na magari ya umeme ya Tasla aliandaa kura ya maoni kwenye mtandao huo akitaka kujua ni wangapi wanataka kurudishwa kwa akaunti ya aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump baada ya kufungiwa miaka miwili iliyopita kutokana na misimamo yake mikali dhidi ya janga la Covid-19 na pia matokeo ya uchaguzi wa Marekani alioshindwa na Joe Biden.

Kombe la dunia kwa mara ya kwanza katika historia litakuwa linafanyika kwenye taifa la Mashariki ya Kati, licha ya chaguo la Qatar kuandaa mashindano hayo kukumbwa na sintofahamu nyingi pamoja na madai ya ufisadi.

Tayari Qatar wametangaza utayarifu wao kuandaa mashindano hayo yanayofuatiliwa pakubwa kote ulimwenguni na moja ya masharti makubwa ambayo yametajwa ni kupigwa marufuku kwa kuuzwa kwa kilevi chochote ndani na nje ya viwanja vyote vitakaoandaa mashindani hayo kwa siku 28 kuanzia Novemba 20.