Senegal yamtema Sadio Mane kutoka kikosi cha kushiriki kombe la dunia

Awali, mchezaji huyo ambaye pia ni nahodha alikuwa amejumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 26 waliokuwa wanaelekea Qatar.

Muhtasari

• Sadio Mane alipata jeraha kwenye mechi baina ya Bayern Munich dhidi ya mahasimu wao Welder Bremen.

• Kocha wa senegal Aliou Cisse sasa atalazimika kupanga timu yake bila Sadio Mane.

Mshambulizi wa Bayern Munich na Senegali, Sadio Mane
Mshambulizi wa Bayern Munich na Senegali, Sadio Mane
Image: Facebook//Sadio Mane

Mwanasoka tajika wa Senega Sadio Mane amendolewa kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwa kushindwa kupona jeraha kwa wakati ufaao.

Hili lilijiri baada ya kupata jeraha la goti lake katika ushindi wa mabao 6-1 baina ya Bayern Munich dhidi ya mahasimu wao Welder Bremen mechi iliyochezwa mapema mwezi huu, jambo ambalo lilitia shaka matumaini yake ya kushiriki kwenye michuano hiyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, aliripotiwa na Shirikisho la soka la Senegal siku ya jumanne Novemba 17 kwamba atakosa kushiriki kwenye mechi baina ya Senegal na Uhoranza inayotarajiwa kuchezwa kwenye mechi ya kundi A siku ya Jumatatu Novemba 21 2022.

"Wakati wa upasuaji, mshipa uliunganishwa tena ila Sadio Mane hatapata nafasi ya kuichezea Senegal kwenye Kombe la Dunia na ataanza kujiuguza mjini Munich siku chache zijazo." shirika hilo lilisema.

Kocha wa mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika Aliou Cisse atamlazimu kupanga timu yake bila nyota huyo muhimu.

Kumpoteza Mane kwenye Kombe la Dunia ni pigo kubwa kwa matumaini ya Senegal nchini Qatar, kwani aliisaidia sana kushinda Kombe la Africa la AFCON mwezi Februari mwaka huu alipofunga penalti ya ushindi kwenye mikwaju ya penalti dhidi ya timu ya Misri kwenye fainali.