(+video) Beki wa Man-City amuuliza Bukaya Saka kama Arsenal itaacha kushinda mechi

Beki Kyle Walker na Bukaya Saka walikutana katika kambi ya timu ya taifa ya Uingereza kujiandaa kwa kipute cha kombe la dunia.

Muhtasari

• Macho yote sasa yanageukia Qatar kwa wiki sita zijazo ambapo Uingereza itacheza na Iran, Wales na Marekani katika Kundi B.

Kambi ya timu ya taifa ya Uingereza ilipasuka kwa vicheko baada ya beki wa kati wa timu ya Manchester City Kyle Walker kutoa ombi la vichekesho kwa mwenzake anayetumikia timu ya Arsenal Bukaya Saka.

Wawili hao walikuwa St. Georges Park kabla ya kuondoka kuelekea Qatar, baada ya kuingia kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji 26 cha Gareth Southgate.

Walker katika video anaonekana akimuuliza Saka iwapo timu ya Arsenal itafikiria kuacha kushinda mechi za ligi kuu, swali ambalo lilikuwa kama la utani hivi na Saka alimjibu kuwa hafai kuwa na hofu juu ya hilo.

Lakini kabla ya mapumziko ya Kombe la Dunia, Saka anatoka katika taji la kushtukiza ambalo limeifanya Arsenal kujinafasi pointi tano mbele ya mabingwa watetezi Man City, na hivyo kuwafanya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2007 kuelekea kwenye sherehe za Krismas wakiwa kileleni mwa jedwali.

The Gunners walishinda Wolves 2-0 wikendi, huku vijana wa Pep Guardiola wakilala kwa 2-1 kwa Brentford.

Kumekuwa na shaka iwapo Arsenal ni wapinzani wa kweli wa taji, huku wadadisi wengi wakiamini kuwa watajikwaa hivi karibuni. Hata hivyo, kikosi cha Mikel Arteta kimezidi kukaza buti kileleni mwa jedwali, na kudondosha pointi tu kwa Manchester United na Southampton msimu huu.

Macho yote sasa yanageukia Qatar kwa wiki sita zijazo ambapo Uingereza itacheza na Iran, Wales na Marekani katika Kundi B.