"Nipasie mpira!" Sadio Mane arudi darasani kujifunza maneno ya msingi ya Kijerumani

Hatua hiyo itarahisisha utumishi wake kwa klabu yake ya Bayern Munich na kuboresha mawasiliano yake uwanjani na wenzake.

Muhtasari

• Mshambuliaji huyo wa Senegal mwenye umri wa miaka 30 anatumia muda wake akiuguza jeraha akisoma Kijerumani akiwa tayari kurejea uwanjani.

Mane akiwa na mwalimu wake wa Kijerumani
Mane akiwa na mwalimu wake wa Kijerumani
Image: Screengrab// YouTube

Staa wa Senegali Sadio Mane ameamua kurudi darasani ili kujifunza Kijerumani kama njia moja ya kurahisisha utumishi wake kwa klabu yake mpya ya Bayern Munichen, miezi kadhaa tangu kujiunga na timu hiyo.

Mane alijiunga na Munich akitokea Liverpool ya Uingereza katika msimu wa majira ya joto mwezi Julai mwaka huu na amekuwa akihangaika kuelewana na wachezaji wenzake uwanjani kufautia tofauti za ndimi na lugha.

Mshambuliaji huyo wa Senegal mwenye umri wa miaka 30 anatumia muda wake akiuguza jeraha akisoma Kijerumani akiwa tayari kurejea uwanjani kwa wababe hao wa Bundesliga.

Katika video hiyo iliyowekwa kwenye kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za Bavarians, Mane anasikika akijifunza maneno ya msingi ya Kijerumani ambayo mchezaji anahitaji uwanjani, ikiwa ni pamoja na 'Tafadhali, pasi mpira' kwa heshima.

Mane kwa sasa hayumo kwenye mchezo wa soka baada ya kuumia kwenye fibula yake ya kulia wakati Bayern ikishinda 6-1 Bundesliga dhidi ya Werder Bremen mnamo Novemba 8.

Mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool, ambaye baadaye alifanyiwa upasuaji, alilazimika kukosa michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar ambapo timu yake ya Senegal ilifika hatua ya 16 bora lakini ikafungwa 3-0 na England.

Tangu ahamie Bayern, Mane amefanikiwa kucheza mechi 14 za ligi kuu na kufunga mabao sita. Alifunga bao lake la kwanza msimu huu katika ushindi wa 6-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt mnamo Agosti 5.

Mane alionekana akiwa na mwalimu wake ambaye alikuwa anamuelekeza katika baadhi ya maneno ya kimsingi kwa lugha ya Kijerumani, yale ambayo aghalabu hutumiwa uwanjani.