Ndovu hatimaye aanguka! Wanabunduki wabanduliwa kileleni

Ushindi wa 3-1 wa Man City dhidi ya The Gunners ugani Emirates uliwafanya wachukue nafasi ya kwanza.

Muhtasari

•Arsenal walishindwa kupata ushindi katika mechi yao ya tatu mfululizo dhidi ya Man City, Jumatano usiku na kuwapelekea kushuka hadi nambari mbili kwenye jedwali.

•Erling Halaand alizima matumaini ya The Gunners kuondoka hata na pointi angalau kwa kuongeza bao la tatu la City katika dakika ya 82. 

Wanabunduki wamebanduliwa kileleni baada ya kuongoza kwa muda mrefu
Image: HISANI

Mbio za ubingwa wa EPL za Arsenal sasa ziko hatarini huku klabu hiyo ikipoteza pointi muhimu katika mechi tatu zilizopita.

Vijana wa Mikel Arteta walishindwa kupata ushindi katika mechi yao ya tatu mfululizo dhidi ya klabu ya Manchester City siku ya Jumatano usiku na kuwapelekea kushuka hadi nambari mbili kwenye jedwali.

Ushindi wa 3-1 wa Man City dhidi ya The Gunners ugani Emirates uliwafanya wachukue nafasi ya kwanza baada ya klabu hiyo yenye maskani yake London kuwa kileleni kwa muda mwingi wa msimu huu wa 2022/23.

Kiungo wa kati matata Kelvin De Bruyne alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 24 kwa shuti kali baada ya kosa la mabeki wa Arsenal. Bukayo Saka hata hivyo aliwasawazishia The Gunners kabla ya kipindi cha mapumziko baada ya mwamuzi Anthony Taylor kuwapa penalti kufuatia kosa la kipa Ederson.

Vijana wa Mikel Arteta walijaribu sana kuwadhibiti mabingwa hao watetezi katika kipindi cha pili cha mchuano huo mgumu lakini kwa bahati mbaya ndoto yao ya kusalia kileleni mwa jedwali la EPL ilikatizwa na bao zuri la Jack Grealish katika dakika ya 72.

Mfungaji bora kufikia sasa, Erling Halaand alizima matumaini ya The Gunners kuondoka hata na pointi angalau kwa kuongeza bao la tatu la City katika dakika ya 82. Wanabunduki wenye kukatishwa tamaa waliendelea kupambana hadi dakika ya mwisho lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kuondoka na chochote kwenye mechi hiyo ya kusahau kwa wachezaji na mashabiki ila huzuni na machozi.

Sasa watatarajia kurejea katika njia zao za ushindi na kuomba kwamba Manchester City na Manchester United waanze kuangusha pointi ili waweze kurejea katika nafasi ya kwanza ambayo wamekaa kwa siku nyingi msimu huu. Wanabunduki pia wana mechi mmoja mkononi ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwao iwapo watashinda.