Maguire aikataa WestHam baada ya kumtongoza, adai anataka kujiunga timu kubwa

Gazeti la Times linadai kuwa ingawa Maguire pia yuko tayari kuondoka Old Trafford, anataka tu kujiunga na 'klabu kubwa' kuliko West Ham.

Muhtasari

• The Red Devils wanadaiwa kutafuta ada ya takriban pauni milioni 40 kwa beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 29.

• Beki huyo alivuliwa unahodha wiki chache zilizopita na kitambaa hicho kukabidhiwa Mreno Bruno Fernandes.

Harry Maguire adhibitisha kupokonywa unahodha wa United.
UNAHODHA Harry Maguire adhibitisha kupokonywa unahodha wa United.
Image: INSTAGRAM

Beki wa kati ya Manchester United, Muingereza Harry Maguire ameripotiwa kuipiga chini posa ya West Ham United kwa madai kwamba timu hiyo si kubwa kwa kiwango anachokitaka yeye.

West Ham United inasemekana kuwasilisha dau la pauni milioni 20 kwa ajili ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza, lakini United waliikataa kwa kuwa ilikuwa chini sana.

Gazeti la Times linadai kuwa ingawa Maguire pia yuko tayari kuondoka Old Trafford, anataka tu kujiunga na 'klabu kubwa' kuliko West Ham.

Kwa bahati mbaya, Wagonga nyundo labda ndio klabu pekee ambayo imeonyesha nia kubwa ya kutaka kumsajili Muingereza huyo, baada ya kuwasiliana na United kuhusu uwezekano wa kumnunua kwa mkopo.

The Red Devils wanadaiwa kutafuta ada ya takriban pauni milioni 40 kwa beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 29.

Beki huyo alivuliwa unahodha wiki chache zilizopita na kitambaa hicho kukabidhiwa Mreno Bruno Fernandes na amekuwa akihusishwa na kuondoka katika timu hiyo.

Taarifa mbali mbali zimekuwa zikidai kwamba Maguire hayuko tena katika mipango na kocha Erik Ten Hag.

Sports Brief wanaripoti kwamba Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza alipata wakati mgumu wa kucheza msimu uliopita chini ya Mholanzi huyo, ambaye alipendelea ushirikiano wa Raphael Varane na Lisandro Martinez katikati ya safu yake ya ulinzi.

Awali kulikuwa na tetesi zilizoihusisha timu ya Chelsea na mchezai huyo ambaye kwa ishara zote hana mustakabali katika timu ya United, lakini tetesi hizo hazikudhibitishwa na pande zote husika.