Mchezaji wa timu ya taifa ya Panama Gilberto auawa kwa risasi

Gilberto Hernández alikuwa amecheza mechi yake ya kwanza katika timu ya taifa ya Panama

Muhtasari
  • Kufikia sasa, zaidi ya watu 50 wameuawa katika mji wa Colón, wenye wakazi 40,000, kwa mwaka huu pekee.

Nyota wa timu ya taifa ya soka ya Panama ameuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Colón. Watu wenye silaha walifyatulia risasi kundi la watu, miongoni mwao Gilberto Hernández mwenye umri wa miaka 26, waliokuwa wamekusanyika katika jengo moja mjini humo.

Hernández alifariki na wengine saba kujeruhiwa katika shambulio hilo. Bado haijabainika iwapo mwanasoka huyo, ambaye pia alichezea Klabu ya Atlético Independiente, ndiye aliyelengwa na shambulio hilo au nia iya washmbuliaji ilikuwa nini.

Kumekuwa na ongezeko la mauaji huko Colón katika muda wa miezi kadhaa iliyopita huku magenge mawili hasimu yakipigania udhibiti wa njia za ulanguzi wa dawa za kulevya.

Kufikia sasa, zaidi ya watu 50 wameuawa katika mji wa Colón, wenye wakazi 40,000, kwa mwaka huu pekee.

Mji wa bandari, kwenye lango la kaskazini la mfereji wa Panama, ni kituo cha kupitisha kokeini inayosafirishwa kwa magendo kutoka Amerika Kusini kupitia Panama hadi Ulaya.

Tukio hilo limetokea Jumapili alasiri kwa saa za huko. Watu wawili wenye silaha walimlazimisha dereva wa teksi kuwapeleka kwenye jengo moja katika kitongoji cha Barrio Norte mjini humo na kuwafyatulia risasi kundi lililokusanyika hapo. Baade walikimbia.

Gilberto Hernández alikuwa amecheza mechi yake ya kwanza katika timu ya taifa ya Panama mwezi Machi mwaka huu katika mechi dhidi ya Guatemala.

Baba ya mchezaji huyo aliwataka vijana wa Colón "kukomesha vurugu", na kutoa wito kwa mamlaka "kuanzisha mipango ya kuwaokoa vijana kutokana na vurugu hizi". Pia aliwataka wauaji kujisalimisha: "Msilete madhara zaidi." Shirikisho la soka la Panama na klabu ya Gilberto Hernández walieleza kusikitishwa na tukio hilo na kutoa rambirambi kwa familia yake.