Vincent Kompany ateuliwa kocha wa Bayern baada ya kushindwa kuiweka Burnley kwenye EPL

Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 38 alitia saini mkataba wa miaka mitatu na Bayern.

Muhtasari

•Kocha huyo wa zamani wa Burnley alibainisha kuwa kusajiliwa na klabu hiyo kubwa ya Ujerumani ni heshima kubwa.

•Anarithi mikoba ya Thomas Tuchel na kuondoka Burnley kwenda Bayern baada ya vilabu hivyo viwili kukubaliana ada ya fidia.

Image: TWITTER// BAYERN MUNICH

Beki wa zamani wa klabu ya Manchester City Vincent Kompany amekabidhiwa jukumu la kuwanoa miamba ya Ujerumani Bayern Munich.

Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 38 alitia saini mkataba wa miaka mitatu na Bayern siku ya Jumatano na ataiongoza timu hiyo hadi Juni 2027.

Akizungumza baada ya uteuzi huo, kocha huyo wa zamani wa Burnley alibainisha kuwa kusajiliwa na klabu hiyo kubwa ya Ujerumani ni heshima kubwa.

"Natazamia changamoto ya FC Bayern. Ni heshima kubwa kuweza kufanya kazi katika klabu hii- FC Bayern ni taasisi ya soka ya kimataifa,” Kompany alisema baada ya kusaini mkataba wake.

Bayern Munich walichukua hatua ya kumteua Kompany kufuatia kuondoka kwa kocha Thomas Tuchel ambaye aliondoka katika klabu hiyo baada ya kumalizika kwa msimu wa 2023/24.

Raia huyo wa Ubelgiji anarithi mikoba ya Thomas Tuchel na kuondoka Burnley kwenda kwa upande wa Bundesliga baada ya vilabu hivyo viwili kukubaliana ada ya fidia, inayoaminika kuwa takriban £10.2m.

Kompany alishinda kombe la Championship na Burnley katika msimu wa 2022-23, lakini Clarets walishuka daraja kutoka kwa Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu uliokamilika baada ya kumaliza katika nafasi ya 19.

Kompany ana uzoefu wa Ligi ya Bundesliga kutoka siku zake za kuchezea klabu ya Hamburg na anajua Kijerumani kwa ufasaha, ingawa uteuzi wake unawakilisha hatua ya ujasiri baada ya Burnley kushuka kutoka Ligi ya Premia.