Euro 2024: Ureno na Ufaransa zafuzu kwa robo fainali ya Euro

Ronaldo alipambana usiku kucha akitafuta bao lake la kwanza kwenye Euro 2024.

Muhtasari

•Ureno walifuzu hadi robo fainali ya Euro 2024 kufuatia ushindi mkubwa 3-0 kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya Slovenia.

Image: BBC

Cristiano Ronaldo alibubujikwa machozi baada ya penalti yake kuokolewa katika muda wa ziada lakini Ureno bado walifuzu hadi robo fainali ya Euro 2024 kufuatia ushindi mkubwa 3-0 kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya Slovenia.

Nahodha huyo nyota wa Ureno alishuhudia penalti yake ikizuiwa na kipa wa Atletico Madrid, Jan Oblak na kufarijiwa na wachezaji wenzake, huku mashabiki wakiimba jina lake uwanjani .

Lakini alipata ahueni na kufunga penalti ya kwanza kwa nchi yake kwenye mkwaju wa penalti - ambapo kipa Diogo Costa aliokoa mikwaju yote mitatu aliyokabili - kabla ya Bernardo Silva wa Manchester City kufunga mkwaju wa ushindi.

Ronaldo alipambana usiku kucha akitafuta bao lake la kwanza kwenye Euro 2024.

Kabla ya penalti yake kuelekezwa kwenye lango, alipoteza nafasi nzuri katika dakika ya mwisho ya muda wa kawaida, akipiga shuti iliyoelekea moja kwa moja hadi kwa Oblak, baada ya krosi zake nyingi kupaa juu ya kichwa chake katika dakika 120 za mchezo mkali.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Bao la kujifunga la Jan Vertonghen liliipeleka Ufaransa katika robo fainali ya Euro 2024 kwa kuishinda Ubelgiji bao moja kwa nunge .

Mchezo ambao haukuwa na ubora na msisimko kwa muda wote ulionekana kupangiwa muda wa ziada, lakini shuti lililopigwa na mchezaji wa akiba Randal Kolo Muani lilimgonga Vertonghen na kuingia kimyani zikiwa zimesalia dakika tano kuhitimisha ushindi huo kwenye Uwanja wa Dusseldorf Arena.

Ufaransa walikuwa wamepoteza nafasi nyingi kabla ya hapo kwani kwa mara nyingine tena kupungua makali kwa timu yao kuliwaangusha, na hata nahodha Kylian Mbappe aliweka juhudi lakini alipiga nje shuti nyingi.