Shabana FC waeleza sababu ya kupunguza idadi ya viti kwenye basi kutoka 52 hadi 36

Klabu hiyo yenye mashabiki wengi haswa kutoka eneo pana la Gusii ilitangaza wiki chache zilizopita kubadilisha mdhamini mkuu kutoka BangBet hadi SportPesa.

Muhtasari

• "Kwa sasa tuna viti 36. Imepunguzwa kutoka 52. Vizuri sana na wasaa,” walitangaza kupitia X.

SHABANA FC
SHABANA FC
Image: SHABANA FC//X

Klabu ya soka ya ligi kuu nchini FKF-PL, Shabana FC wamefichua mabadiliko mapya kwenye basi la timu huku wiki ya pili ya mechi ya ligi msimu huu zikitarajiwa kuendelea.

Kupitia ukurasa wao wa X, zamani ukijulikana kama Twitter, Shabana FC walifichua kwamba kwa kushirikiana na mdhamini wao mpya ambaye ni SportPesa, wamemaua kufanyia basi la timu mabadiliko chanya ili kuwapa wachezaji starehe wanaposafiri kote nchini kwa ajili ya mechi za mzunguko wa FKF.

Klabu hiyo ilifichua kwamba ni kutokana na dhana hii ya kuweka maslahi ya wachezaji mbele ambapo wameamua kupunguza idadi ya viti kwenye basi hilo kutoka 52 hadi 36 ili kufanya usafiri kuwa wa starehe zaidi bila kufinyana.

“Kama tulivyoahidi mapema, ili kuhakikisha wachezaji wetu na wafanyakazi wa makocha wanasafiri kwa raha, tumeshirikiana na mshirika wetu mkuu, SportPesa, kukarabati mambo ya ndani na nje ya basi la timu yetu.”

“Mpango huu ni sehemu ya juhudi zetu zinazoendelea za kuanzisha utambulisho mahususi wa chapa. Kwa sasa tuna viti 36. Imepunguzwa kutoka 52. Vizuri sana na wasaa,” walitangaza kupitia X.

Klabu hiyo yenye mashabiki wengi haswa kutoka eneo pana la Gusii ilitangaza wiki chache zilizopita kubadilisha mdhamini mkuu kutoka BangBet hadi SportPesa, msimu mmoja baada ya kurejea kwenye ligi ya FKF baada ya kuwa kibaridini kwa muda wa miaka 17.