Picha ya Messi akiwa na Kombe la Dunia ndiyo imependwa zaidi kwenye Instagram

Posti hiyo imepiku likes 57,000,000 na kuvunja rekodi ya awali.

Muhtasari

•Posti hiyo ya Messi ilikuwa imependezwa mara 57, 163, 000 kwenye Instagram kufikia kuchapishwa kwa makala haya.

•Messi alisherehekea ushindi wa timu yake na kueleza jinsi ilvyokuwa ndoto yake kubwa kutwaa Kombe la Dunia

Image: INSTAGRAM// LIONEL MESSI

Mshambuliaji matata wa Argentina Lionel Messi  ameweka rekodi mpya kwenye Instagram baada ya posti yake ya hivi majuzi kupata likes nyingi zaidi kuwahi kupatikana kwenye mtandao huo wa kijamii.

Posti ya mchezaji huyo wa PSG akiwa ameshika Kombe la Dunia kufuatia ushindi wa Argentina siku ya Jumapili imepiku likes 57,000,000 na kuvunja rekodi ya awali iliyokuwa imeshikiliwa na akaunti ya 'The World Egg'.

Katika chapisho hilo lake la Jumatatu, Messi alisherehekea ushindi wa timu yake na kueleza jinsi ilvyokuwa ndoto yake kubwa kutwaa Kombe la Dunia

"MABINGWA WA DUNIA!!!!!!! 🌎🏆 Mara nyingi sana niliota, nilitamani sana hata sijaanguka, siwezi kuamini," alisema.

"Asante sana kwa familia yangu, kwa wote wanaoniunga mkono na pia kwa wote waliotuamini. Tunathibitisha kwa mara nyingine kwamba Waajentina tunapopigana pamoja na kuungana tunaweza kufikia kile tunacholenga. Sifa ni ya kundi hili ambalo liko juu ya mtu mmoja, ni nguvu ya wote kupigania ndoto ileile ambayo pia ilikuwa ni ya Waargentina wote. Tulifanya hivyo!!!," alisema mshambuliaji huyo.

Posti hiyo ya Messi ilikuwa imependezwa mara 57, 163, 000 kwenye Instagram kufikia kuchapishwa kwa makala haya.

Hapo awali rekodi ya posti pendwa zaidi kwenye Instagram ilishikiliwa na akaunti ya 'The World Egg.'

Katika chapisho hilo la pekee kwenye ukurasa huo, mchapishaji alikuwa amewaomba watumiaji wa Instagram kukusanyika pamoja na kusaidia kuvunja rekodi ya awali ya likes milioni 18 iliyokuwa imewekwa na Kylie Jenner.

"Wacha tuweke rekodi ya ulimwengu pamoja na tupate chapisho linalopendwa zaidi kwenye Instagram. Tukishinda rekodi ya sasa ya dunia inayoshikiliwa na Kylie Jenner (milioni 18)! Tuko na hii 🙌," chapisho hilo la Januari 2019 lilisoma.

Kufikia sasa Messi ni mchezaji wa pili mwenye wafuasi wengi zaidi kwenye Instagram  (402M), nyuma ya Christiano Ronaldo (519M).