Tottenham wamtimua kocha baada ya kupewa kichapo cha mbwa na Newcastle, 6-1

Levy alitangaza kuwa Ryan Mason atajaza nafasi hiyo mara moja.

Muhtasari

•Mwenyekiti wa klabu, Daniel Levy alitangaza kwamba Stellini ameondoka pamoja na kikosi chake cha wakufunzi.

•Alisema yeye, bodi, makocha na wachezaji ni wa kulaumiwa kwa matokeo hayo hafifu ambayo alisema hayakubaliki.

ametimuliwa kama kocha wa Tottenham.
Christian Stellini ametimuliwa kama kocha wa Tottenham.
Image: HISANI

Klabu ya Tottenham ilimtimua kocha wa muda Cristian  Stellini siku ya Jumatatu, takriban mwezi mmoja tu baada ya kuchukua hicho.

Jumatatu jioni, mwenyekiti Daniel Levy alitangaza kwamba Stellini ameondoka pamoja na kikosi chake cha wakufunzi na kufuatia hayo akawashukuru kwa kazi ambayo walifanya katika kipindi cha mwezi mmoja ambao umepita.

"Cristian alichukua usukani wakati mgumu wa msimu wetu na ninataka kumshukuru kwa njia ya kitaalamu ambayo yeye na wakufunzi wake wamejiendesha wakati wa changamoto kama hii. Tunawatakia heri," alisema katika taarifa.

Wakati huo, Levy alitangaza kuwa aliyekuwa kocha wa muda wa klabu hiyo mwaka wa 2021, Ryan Mason atajaza nafasi hiyo mara moja.

"Ryan anaijua Klabu na wachezaji vizuri. Tutatoa taarifa zaidi juu ya wakufunzi wake kwa wakati ufaao," aliongeza.

Mwenyekiti huyo alisikita kuhusu matokeo ya Jumapili dhidi ya Newcastle ambapo klabu hiyo ilipokea kichapo cha mbwa cha 6-1, huku wakifungwa mabao matano ya kwanza chini ya dakika 21 pekee.

Alisema yeye, bodi, makocha na wachezaji ni wa kulaumiwa kwa matokeo hayo hafifu ambayo alisema hayakubaliki.

"Ilikuwa ya kusikitisha kuona. Tunaweza kuangalia sababu nyingi kwa nini ilitokea na ni wakati mimi, Bodi, makocha na wachezaji lazima tuchukue jukumu la pamoja, hatimaye jukumu ni langu," alisema.

Stellini alichukua usimamizi wa klabu hiyo baada ya aliyekuwa kocha mkuu, Antonio Conte kutimuliwa takriban mwezi mmoja uliopita.

Tottenham ilitamatisha mkataba wake na Conte baada ya Muitaliano huyo  kuishambulia klabu hiyo na wachezaji wake.

Hapo awali, Conte ambaye alikuwa akiisimamia klabu hiyo yenye maskani yake London tangu Novemba 2021 aliwakashifu wachezaji wake akiwaita "wabinafsi" baada ya kutoka sare ya 3-3 na Southampton.

Mnamo Machi 26, Tottenham kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya klabu hiyo ilitangaza kwamba meneja huyo mwenye umri wa miaka 53 ameondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili.