Moses Kuria kumpigia debe mgombeaji wa ODM - Kibra

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amesema atamuunga mkono mgombeaji wa ODM Benson Musungu ikiwa atateuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kwa kiti cha eneo bunge la Kibra.

Musungu ni miongoni mwa wagombeaji 11 wanaotaka tikiti ya ODM katika uchaguzi huo mdogo.

ODM imepangiwa kuandaa uteuzi wa atakaye peperusha bendera yake Jumamosi hii baada ya kuahirisha zoezi hilo kutokana na changamoto za kiusalama kwa sababu polisi wengi walikuwa wanashiriki shughuli ya kuhesabu watu.

Katika Facebook, Kuria alisema atamuunga mkono Musungu kwa sababu yeye ni mzaliwa wa Kibra huku akimfananisha na aliyekuwa mbunge wa eneo hilo marehemu Ken Okoth. Alisema kwamba kiongozi aliyezaliwa Kibra anafahamu shida na changamoto za wakaazi wa eneo hilo na ana nafasi nzuri kuboresha maisha ya watu wa eneo hilo.

"Rafikiyangu Ken Okoth alizaliwa Kibra na alikuwa amejitolea sana kuimarisha maisha ya watu wa Kibra. Mtu ambaye nitapigia debe kuendeleza mipango ya Okoth ni mzaliwa mwingine wa eneo hilo, Benson Musungu," Kuria alisema

Matamshi yake yanajiri siku mbili tu baada ya aliyekuwa mchezaji wa kimatiafa wa Harambee Stars McDonald Mariga kuteuliwa kupeperusha tiketi ya Jubilee katika uchaguzi huo mdogo wa Novemba tarehe 7.

Mariga anasemekana kushinikizwa na Naibu Rais William Ruto, madai ambayo aliyakanusha siku ya Jumatatu baada ya kupewa tiketi ya chama hicho. Kuria kupitia twitter siku ya Jumatatu alimtaka Ruto kumwacha Mariga aendelee kucheza mpira na kuimua talanta za vijana badala ya kujiingiza katika taaluma chafu ya siasa.