Msichana aliye ozwa kwa mzee wa miaka 50 aokolewa

Msichana wa kike mwenye umri wa miaka 11 ambaye alikuwa ameozwa kwa mzee wa miaka 50 katika kijiji cha Barsaloi Samburu ameokolewa.

Mtoto huyo aliokolewa kwa njia ya kisiri na nduguye mkuu baada ya kugundua alikuwa ameozwa na wazazi wake.

Kijana huyo wa kidato cha tatu alikutana na dadake katika kituo cha kibiashara cha Barsaloi baada ya masaa ya shule na alipotaka kujua mbona hakuwa shuleni alimwambia kuwa yeye ni mke wa mtu.

"Nilijua hilo sio jambo nzuri na nikaamua kumuokoa. Mzee huyo sio wa kuaminika kitabia kwani ameishi Mombasa." Nduguye alisema.

OCPD wa Samburu ya kati Alex Rotich alisema kuwa nduguye yule mtoto alipigia simu shirika la wasichana la Samburu (SGF) ambao walimsaidia kumuokoa dadake.

"Tunamtafuta yule mzee pamoja na wazazi wa yule msichana ili wawajibikie makosa yao." Alisema.

Mkuu huyo wa polisi aliwarai wakazi kutojihusisha na desturi ambazo zinaleta madhara.

Aliongeza kuwa serikali haitaonesha huruma kwa mzee huyo ambaye alikuwa tayari ameanza kulipa mahari kwa familia ya mtoto yule.

Pascalina Naibash anayefanya kazi na Samburu Girls Foundation alimpongeza ndugu yule kwa kumuokoa dadake akisema kuwa pia wasichana wana haki ya kupewa fursa sawa kama vijana.

"Msichana yule hajawahi pelekwa shuleni lakini ndugu zake wote wako shuleni, pamoja na aliyemuokoa. Hii ndio vita ambayo sisi hupigania kila siku." Naibash alisema.

-Martin Fundi