Must Read: Still Single?Sababu 8 zinazokufanya usiwe na Mpenzi

Wandia Kamau
Wandia Kamau
Mara sio moja umesikia  msemo huu ‘ maisha ni mafupi’.Je ushawaji kujiuliza mbona binadamu hutaka maisha yawe marefemu ?  Wengi wanajishughulisha na vingi ili kujiridhisha ,lakini hadi  leo hakuna kitu   ambacho huwapiga watu chenga kama mapenzi.Mapenzi humfanya hata mtu  anayeonekana kuwa na uthabiti fulani au talanta au umaarufu kuonekana kama mtoto .Mapenzi  yamefahamika kuwafanya hata  walio na maamlala kuanzisha vita na taifa au ufalme jirani . Mapenzi yamefanya watu kuua . In short,Mapenzi  yanarun dunia !

Lakini basi kama mapenzi ni kitu kizuri mbona kuna watu ambao hukosa au hushindwa kupata wapenzi ? Nakubali kwamba kuna watu ambao wenyewe huamua kusalia single ,wana sababu zao na ni busara kuziheshimu .  Wanaolengwa hapa ni wale ambao wanataka kuwa katika uhusiano lakini wamefeli,wamekosa kupata  wenzao au wameshindwa kudumisha uhusiano.

Hizi ni baadhi ya sababu ambazo  huenda zinakufanya unasalia kuwa Single .

  1.Kuogopa  kuvunjwa moyo

Aghalabu  wengi  hutumia historia ya masaibu ya kale waliopitia kuamua mkondo wa hatua na maamuzi yao .Kwa sababu uliwahi kuvunjwa moyo mara moja au kushuhudia unayemjua akiteswa  moyo na masuala ya mapenzi  usije ukajitia katika kisanduku cha upweke  kwa sababu ya hilo .Wengi hukutana  na kutangamana na watu ambao wanaafikia maazimio yao ya uhusiano  ila kwa sababu ya woga wa kitakachofuatia ,wanajipata   wamebanwa na hofu na kusalia kimya . Umeskia na kusoma zaidi ya mara moja kwamba  ‘Nilipenda mara moja na nikafadhaishwa kwa hivyo ,siwezo kupenda tena’. Upuuzi! Maisha hayawezi kuelekezwa  na  wimbi la hofu kila wakati . Wanaofaulu katika lolote ni wajasiri na hata wakiangushwa mara moja ,safari yao huanza tena upya.

2.Kutojiamini

 ‘Self esteem’. Jambo hili huanza unapobalaghe wakati maungo yako na maumbile yanapoanza kubadilika .Maajuzi  nimekutana na mwanadada mrembo wa  kutisha ,ila mtoto wa kike ameniambia   kwa upole na huruma kwamba hawezi kuvalia rinda! Sababu? Eti rafiki zake walimwambia kwamba umbo lake sio zuri akivalia rinda.Argh. Hiki kimemfanya maskini Naomi hajiamini machoni pa wanaume akiwa amevalia rinda .Anafikiria hapendezi na kumbe kauli ya rafiki zake ilikuwa potovu .Vitu vichache na dhana  zisizo na msingi ni baadhi ya vinavyotufanya tukose kujiamini . Najua hakuna aliye na uhalisi . No One is perfect ! lakini jamani usije ukajizika kwa sababu ya kukosa kujiamini kwa lolote . Kuna watu ,wanawake kwa wanaume wanaofikiri kwamba hawana hadhi ama uwezo wa kupenda au kupendwa na mtu fulani .Jipe fursa  angalau !

3.Kutojijua

 Hili ni zito .Jamani hakikisha kwamba unajifahamu kibinafsi .uwezo wako ni upi .Mchango wako katika uhusiano wowote ni upi ? mtazamo wako kuhusu kila jambo ni upi? Ni vipi unajibeba ukiwa faraghani na unapokuwa hadharani? Ni nyakati gani za kusema ukweli na ni zipi  za kutumia chembe ndogo  za urongo ? Ni mipaka ipi unaweza kujizuia kufanya kisichofaa? Hakikisha kwamba unajifahamu kwa undani  kabla ya kutaka uhusiano .Watu wengi hawajijui ndiposa wakati wanapoanza  uhusiano ,haufaulu kwa ajili mwenzao huwaambia  vitu tofauti sana . Najua ushawahi kusikia kauli hii  ya kiingereza-‘S/h’es  Not the Person I knew’. Hili hutokana na mtu kutojijua au kutoa taswira isio  halisi .Unapokutana na mtu ,kuwa mkweli,kuwa halisi ,kuwa muwazi kuanzia mwanzo .Usije ukamkanganya mwenzako kwa kutoa  picha mbili tofauti za ubinafsi wako.Be Real !

 

  1. Kuchagua/Maringo/ubaguzi/

 Sitawafichua wote naowajua ambao waliachwa  vinyua wazi hadi leo kwa ajili ya  tabia yao ya kutoona uzuri katika kila kitu . Namjua mtu ambaye alitimu umri wa kuolewa lakini kila   mvulana aliyekuja kutoa posa alipatikana kuwa na kasoro .  Zeina  hakukosa kasoro katika kila mwanamme aliyemtaka ..Mara oh... huyu Selemani ana kichwa kikubwa….  Huyu Adamu mzuri kweli ana bidii lakini ni mfupi …… eh ...huyu  Charles  mtanashati kweli  lakini ni mweusi …mara  huyu  Peter ananipendeza lakini  ni maskini hohe hahe..na orodha ikawa ndefu zaidi ..na hata sijazidisha chumvi kwa hili .True story .  Najua kila mtu ana  vigezo anavyoangalia katika mtu anayetamania awe mchumba au mpenzi wake .Lakini basi itakuwa makosa endapo kila sababu yoyote hata iwe nyepesi kama   nyuzi kuchukuliwa kuwa kitu kikubwa na kukukosesha fursa . Fahamu kwamba kuna vitu ambavyo unaweza  kuishi vyema navyo. Kila unachoona ,hukioni kilivyo-unaona kasoro tu..unanusa udhaifu 100 metres away!

  1. Kuogopa Ushindani

 Kuna wasiokuwa na wapenzi kwa sababu ya kuhofia ushidani .Je nikimpenda mtu na kumbe kuna mwengine anayempenda ,nitaweza kumnyakua? Karne hii ,kuna ongezeko na uwezekano mkubwa wa kujipata katika  ninachokiita   ‘Relationship food chain’ –unakuwa sehemu ya sakata  kubwa ya uhusiano na mtu ambaye ana uhusiano kama huo na watu wengine kadhaa.Mwishowe unasalia kuwa tu sehemu ya   muundo mkubwa wa mduara unaozunguka kuanzia Januari hadi Disemba  bila matokeo ya kuonekana . Kuna  wanaoogopa kujipata katika visa kama hivyo vya mapenzi .wanaogopa ushindani uliopo. Kuna  mwanamke ambaye hawezi kukubali kwamba mumewe au mchumbake anawavutia pia watu wengine nje .Kuna mwanamme ambaye hawezi kamwe kukubali kwamba mchumbake anawavutia wanaume wengine .Wakati mwingine kufahamu hatari kama hizo katika mahusiano pia huwafanya watu kuamua kuwa single . Lakini iwapo utakuwa mkweli kuanzia mwanzo katika uhusiano wako na ujifahamu,basi huwezi kukosa mtu wa kumpenda  kwa sababu ya kuogopa ushindani .Usisalimu amri  haraka .

6.Kujitenga/kujiweka pembeni

Umekuwa na mtindo fulani ambao sasa unaweza kutabirika .Mtindo wako wa  kuanzia jumatatu  hadi  jumapili unajulikana na hufanyi kipya ili kujiuza kama anayehitaji au kutaka uhusiano . umejitenga   na hutangamani na  hata wadudu! Kila chako  ni wewe pekee yako!  You are riding solo .Itakuwa vigumu sana  kupata mtu au kuingia katika uhusiano  endapo   hii ndio sababu inayokuzuia kuwa katika uhusiano . Kuwa na marafiki ,hudhuria hafla  hata zisizohusiana na kazi yako . ‘funua fikra’ na uwe  tayari  kujithubutu kuwajua watu wapya na wenye mitazamo tofauti na wako. Shiriki  michezo au shughuli ambazo ni ngeni kwako ,kubali  vipya na kuwa tayari kucheshwa na yalio tofauti .

7.Kujibana kutumia  vijikanuni vyetu

Kutafuta mapenzi sio kibarua rahisi ,lakini   ni  vizuri kujianzia safari hii mwenyewe ili unachoona na kuhisi kiwe ni kutoka kwako . sio cha kuambiwa . ni vizuri kuziepuka tabia au dhana ambazo zimekuwa zinakuzuia kujiacha nje . Mitindo na vijikanuni ambavyo umevitunga kuendesha maisha yako vinaweza kuwa vikwazo vikubwa  kwako kupata mtu anayekupenda . Usiogope kuumizwa .Sote tuna  udhaifu  ,ambao mara nying hudhihirika bayana tunapoanza kumsongea mtu na kumpenda . Kwa hivyo kuafikia kilele cha mapenzi  ni safari ya wajasiri  na inaridisha sana  kwa ajii ya nguvu na kujituma ambako tunadhihirisha ili kupendwa  na mtu au kumpenda mtu .  Huwezi  kujua unajipenda vipi endapo hujawaji kujipa fursa ya kumpenda mtu .Uhusiano wako na mtu  mwingine tofauti hujenga Uthabiti wa kindani wa uhusiano wako na wewe mwenyewe.Love somebody..Please

8.Kutaka vya rahisi /vyepesi

Kwa wakati mwingine ,mambo tuliopitia hutufanya kuwa wavivu kupigania chochote .Hali hii hutufanya tujiambie kwamba kuna njia rahisi ya kumfanya mtu kukupenda .lakini ukweli ni kuwa  chochote cha kupata kwa urahisi hakidumu . Uhusiano wowote wa kudumu huchukua muda na ni kazi  nzito. Huhitaji  kujitolea  na  uvumilivu .Vyote hivi ni vigumu na hivyo basi wengi hujipata  na jaribio la kutumia mkato kupendwa . Usiseme wongo; wongo baadaye utakurudi . Usiwe na matarajio kupindukia au  yasioweza kuafikiwa-hili litakufanya umchukie mwenzako na kukufanya kutoweza kuwa katika uhusiano .Usikimbilie uhusiano na mtu bila kumfahamu . Wengi hukimbilia ‘vivutio’. Kila mtu ana sifa au mambo  yanayomfanya kuwavutia watu kwa nje lakini huenda siye mtu halisi wa kuwa katika uhusiano naye . Njia hizi za mkato na rahisi zinakufanya unajiingiza katika mahusiano yasiokufaa kisha baadaye unafoka kwa   ukali maneno kama ‘All men are the same’.Dada ,kwani ulipewa kazi ya kupima sampuli zote za wanaume au ulitaka mapenzi?