Mwanamke anayefuga konokono aliyetengwa akishukiwa kuwa na covid 19

Wangui Waweru anapokumbuka mchana wa tarehe 26 mwezi Machi mwaka huu hulazimika kujizuia sana kulia kutokana na maisha yake yalivyobadilika siku hiyo.Kabla ya siku hiyo, maisha yake yalikuwa ya kawaida tu na alikuwa na marafiki wengi. Lakini wapo marafiki wa dhati, na wanaoyeyuka wakati wa shida.

Siku hiyo, gari la kuwabeba wagonjwa lilifika nyumbani kwake kumchukua. Hii ni baada yake kujihisi kana kwamba alikuwa ameambukizwa virusi vya corona.Gari hilo lilipoingia kwenye boma lao kumsafirisha hadi hospitalini, marafiki zake na baadhi ya majirani walianza kuzungumzia tukio hilo. Taarifa za kuchukuliwa kwake na maafisa wa afya zikaenea kama moto wa nyikani.

Taarifa zilibuniwa , zikapikwa na kutiwa chumvi chumvi.

"Ni vigumu kusahau yaliyonitokea baada ya kubebwa na gari la wagonjwa mahututi hadi hospitalini. Kumbe niliacha minong'ono ya kila aina kule kijijini mwangu. Watu walieneza uvumi jinsi nilivyodhoofishwa na ugonjwa wa corona," anasema.

"Cha ajabu ni kuwa rafiki yangu wa karibu, niliyekuwa namueleza kuhusu dalili zangu ndiye aliyenisaliti zaidi kwa kunisemasema hapa na pale," Wangui anakumbuka .

 

Kwa kipindi cha siku 7 hivi kabla ya kisa hicho, mwanadada huyu alikuwa karantini akiwa nyumbani kwake, mtaa wa Lanet katika Kaunti ya Nakuru. Alipoamka siku hiyo, kipimo cha joto mwilini kilikuwa kimepanda sana kuliko kawaida na kuwa nyuzi 41.2.

Kawaida binadamu huwa na kipimo cha 37. Vile vile alijihisi kuishiwa na nguvu na pia alikuwa na homa kali.

Kutokana na dalili hizo, alikuwa na wasiwasi sana kwamba alikuwa ameambukizwa virusi hiyo.

Ni yeye mwenyewe aliyewaita wahudumu wa hospitali moja mjini Nakuru na kuwaeleza kuhusu dalili zake.

Kulingana na Wangui, wahudumu wa afya walimshauri dhidi ya kusafiri na magari ya umma, bodaboda au teksi.

Njia pekee ilikuwa gari la kuwabebea wagonjwa. Gari hilo hakujua kwamba lingekuwa chanzo cha unyanyapaa.

Wanakijiji walipoliona gari hilo, huku wahudumu wakiwa wamevalia vifaa kinga, basi uvumi ukaenea mno kuhusiana na jirani yao kuwa muathirika wa corona.Kulingana na mwanadada huyu, wengi ni wale waliohisi kuwa angekuwa chanzo cha kueneza ugonjwa huo maeneo yao, kama hakuwa ameshafanya hivyo tayari.

"Wakati huu ambapo dunia inapigana na corona, sijui ni kutokana na uelewa duni wa corona au ni vipi. Nimepitia hali ngumu mno. Unapodhaniwa una corona unaonekana kana kwamba hufai kukaa karibu na watu, " alisimulia Wangui

Wangui huwa mkulima wa konokono, kazi ambayo si wengi wanaojihusisha nayo. Mwanadada huyu anasema kuwa kutoka zamani kutokana na yeye kujitosa kwenye kazi ya konokono baadhi ya watu walijitenga naye.