Nchi za Afrika ambazo huenda raia wake wakapigwa marufuku kuingia Marekani

Raia wa nchi nne za Afrika ikiwemo Tanzania huenda wakapigwa marufuku kuingia nchini Marekani, vyombo vya habari vinaripoti.

Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vimeripoti kuiona orodha ya nchi hizo ambayo inaweza kuwekwa wazi na serikali ya nchi hiyo Jumatatu ijayo, Januari 27.

Nchi nyingine za Afrika kwa mujibu wa ripoti hizo ni Nigeria, Sudan na Eritrea.

Rais wa Marekani, Donald Trump akiwa Davos nchini Uswizi amelithibitishia gazeti la Wall Street Journal kuwa ana mpango wa kuongeza idadi ya nchi kwenye orodha ya katazo la kuingia Marekani, lakini aligoma kuzitaja nchi hizo.

Kwa mujibu wa gazeti la Politico, rasimu ya nchi hizo bado haijakuwa rasmi na inaweza kubadilishwa.

Magazeti hayo pia, likiwemo la New York Times yanaripoti kuwa bado kuna mabishano baina ya maafisa wa Ikulu ya White House juu ya kujumuishwa ama kutolewa kwa nchi moja au mbili kwenye orodha hiyo.

Nchi nyengine nje ya Afrika ambazo zinasadikiwa kuwemo kwenye rasimu hiyo ni Belarus, Myanmar na Kyrgyzstan.

Katazo hilo halitarajiwi kuwa la moja kwa moja ama kuathiri kila mtu bali aina fulani ya viza ama vinaweza kuwalenga maafisa wa serikali.

Licha ya vyombo hivyo vya Marekani kuitaja Tanzania lakini vyote havijaeleza kwa nini taifa hilo la Afrika Mashariki limo kwenye rasimu ya orodha.

-BBC