Wizara ya mashauri ya kigeni nchini imeitaka Somalia na mashirika ya kimataifa kuchunguza kikamilifu kuanguka kwa ndege moja ya kampuni ya kibinafsi iliyokuwa ikisafirisha misaada ya kupambana na virusi vya corona.
Ndege hiyo ilianguka katika hali ya kutatanisha katika eneo la Bardale, Baidoa nchini Somalia siku ya Jumatatu tarehe 4. Kenya imeyataka mashirika mengine ya ndege yanayohudumu katika eneo hilo kuchukua tahadhari kwani hali iliyosababisha ajali ya ndege hiyo bado haijaeleweka .
Wizara ya mashauri ya kigeni ya Kenya imesema itashirikiana na mashirika mengine kufuatilia kwa karibu uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na kutafuta suluhisho. Ndege hiyo yenye nambari ya usajili 5Y-AXO ilikuwa ya kampuni ya African Express na ilisababisha vifo vya watu wote sita waliokuwemo .