'Nia yangu ilikuwa kuwanyamazisha mahasidi!' Asema bingwa Kipruto

kipruto
kipruto
Mshindi wa mbio za mita elfu 3 kuruka viunzi duniani Conceslus Kipruto, anadai kuwa nia yake ilikua kuwanyamazisha mahasidi waliodai kuwa Kenya ingepoteza mbio hizo.  Kipruto ambaye ni mmoja kati ya washindi wa medali tano za dhahabu, sasa anawania kushinda nyingine katika mbio za olimpiki mwaka ujao. Timu ya Kenya iliwasili nchini jana kutoka Doha, Qatar baada ya kunyakua jumla ya medali 11.

Timu hiyo ililakiwa na waziri wa michezo Amina Mohammed katika uwanja wa JKIA. Waziri Amina alikipongeza kikosi hicho kwa jitihada zao, kujitolea na nidhamu iliyopelekea Kenya kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Marekani.

Hayo yakijiri, rais wa kamati ya kitaifa ya Olimpiki nchini Paul Tergat ameteuliwa kwenye kitengo kipya cha kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC, cha tume ya waandalizi wa siku za baadaye kama mwanachama anayewakilisha kamati za kitaifa. Tume hiyo chini ya usimamizi wa raia wa Norway Kristin Kloster itatoa ushauri na mapendekezo kwa bodi kuu ya IOC kuhusiana na waandalizi wa Olimpiki za misimu ya joto na baridi pamoja na michezo ya Olimpiki kwa vijana.

Tukifika ulaya, Arsene Wenger amethibitisha anatathmini kuchukua wadhfa wa kiufundi katika shirikisho la FIFA, lakini anasema haitamzuia kuregea katika umeneja. Raia huyo wa Ufaransa amekua bila kazi tangia Mei mwaka uliopita wakati ajira yake ya miaka 22 Arsenal ilipotamatika. Wenger ambaye atatimiza miaka 70 mwezi huu, hajaamua hatua atakayoichukua baada ya kukataa ofa za kusimamia ligi ya Primia.

 Kipa wa Tottenham Hugo Lloris atakosa muda wa msimu wa mwaka 2019 uliosalia kutokana na jeraha la mkono, alilolipata wakati wa mechi yao ya ligi ya Primia waliyopoteza 3-0 kwa Brighton. Nahodha huyo mfaransa na mshindi wa kombe la dunia mwaka 2018 hatarajiwi kufanya mazoezi hadi mwaka ujao, lakini hatafanyiwa upasuaji.

Lloris alianguka vibaya alipokua akijaribu kuushika mkiki wa Neal Maupay. Paulo Gazzaniga atachukua mahala pake hadi atakaporegea.