Nilikua mnywaji mkubwa wa pombe kwa miaka 20, Jaji Mkuu Maraga afichua

Jaji mkuu David Maraga, amewashauri vijana wenye uraibu wa mihadarati kutafuta usaidizi kwa wataalamu au kutoka kwa Mungu.

Alipokua akizindua Kampeni ya Uhamasisho kuhusu mihadarati Jumamosi katika Chuo Kikuu cha JKUAT, Maraga amekiri kwamba miaka 20 ya maisha ilipotea kwa ulevi.

'Nilibatizwa Oktoba tarehe 30 mwaka wa 1965 nikiwa bado katika shule ya msingi lakini nikapata marafiki wa kupotosha nikiwa shule ya upili. Wakati mwingine hata nilikunywa kwa mkopo' Maraga alisema.

Maraga alisema bado alikunywa pombe kupita kiasi alipokua katika chuo kikuu na hata wakati alipoanza tajriba yake ya uanasheria.

'Kwa zaidi ya miaka 20 sikuwa na maendeleo yoyote maishani kwa ajili ya pombe. Ningeenda nyumbani saa tisa alfajiri na kuitisha chakula. Mke wangu angeniuliza iwapo kweli ilikua chakula cha usiku au kiamsha kinywa nilichotaka. Singekua Jaji Mkuu iwapo singemgeukia na kumfuata Yesu Kristo' alisema.

Maraga amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu kujizatiti katika vita dhidi ya mihadarati kwani jamii kwa sasa inawaruhusu walanguzi kuishi miongoni mwai na kuifanya kuwa rahisi kupata mihadarati.

“Kwa kupenda pesa, walanguzi wanawauzia watu mihadarati na kusababisha uraibu huo kuwa miongoni mwa changamoto kuu zinazoikumba nchi hii.

Jaji mkuu amelalama kwamba licha ya sheria zilizopo zinazonuiwa kuthibiti ulanguzi wa mihadarati, uraibu huo bado unazidi kuongezeka.

Katika hotuba yake Maraga amefichua athari za utumizi wa mihadarati miongoni mwa vijana.

Hii ni pamoja na kudorora kwa masomo na kuwa na fikra za kujitoa uhai, ukosefu wa ajira, umaskini na maradhi ya akili na kisakolojia.