Mjane wa Ken Okoth kurithiwa na kakake mumewe - Wazee wa waluo wadai

Luo.elders
Luo.elders
Mjane wa marehemu mbunge wa Kibra Ken Okoth, Monica, anafaa kwanza kufanyiwa tambiko ili kumsafisha kabla ya kuthiwa na kaka mkubwa wa marehemu mumewe, wazee wa jamii ya waluo wamesema.

Mwenyekiti wa wazee hao Nyandika Ongadi katika mahojiano ya kipekee na gazeti la The Star alisema kwamba Monica anafaa kwanza kufika nyumbani kwao Okoth eneo la Kasewe, Kaunti ya Homa Bay kwa tambiko za kusafishwa.

"Ikiwa ni ukweli Monica ni mke wa Okoth anafaa kutii mila za jamii ya mumuwe,” alisema.

Kusafishwa, kulingana na wazee wa Luo, kunahusisha kushiriki tendo la ndoa bila kinga na ‘msafishaji’.

Msafishaji, Ongadi alisema, huwa mtu asiyekuwa na uhusiano na marehemu.

"Monica atakapofika atafanyiwa vipimo kubaini hali yake ya HIV na maradhi ya zinaa kabla ya msafishaji kuanza kazi yake," Ongadi alisema.

Mzee huo alisema kwamba tambiko za kusaofisha ni muhimu sana kuondoa laana ambazo mjane anaaminika kupata kutokana na kifo cha mumewe.  Baada ya ‘kusafishwa’ mjane anatarajiwa kurithiwa na kakake Okoth na kujengewa nyumba (Simba) au boma.

“Ni hiari ya kakake Okoth anayetaka kumrithi. Ikiwa hapatakuwepo na kakake anayetaka kumrithi basi jamaa mwingine wa ukoo wake anaweza kukamilisha tamaduni za jamii ya waluo kwa kumrithi,” Ongadi alisema.

Ongadi pia alisema kwamba Monica anafaa kuzuru nyumbani kwao Okoth ili kufanyiwa tambiko na mila za waluo pamoja na familia yake.

“Tambiko kama vile kula pamoja na familia ya marehemu bwanake nyumbani ni muhimu sana. Familia itazika mgomba nyumbani kama ishara ya kuzikwa kwake,” Ongadi alisema.

Mamake Okoth anatarajiwa kutoa taarifa kuhusiana na swala la tamaduni za waluo atakaporejea jijini Nairobi.

Okoth alifariki kutokana na saratani ya utumbo Ijumaa iliyopita katika Nairobi Hospital.

Mwili wake ulichomwa siku ya Jumamosi asubuhi katika makaburi ya Kariokor Nairobi.