Njia Panda? Je,Kenya itachukua hatua gani huku mataifa mengine yakilegeza vikwazo na mengine yakikaza kamba kuhusu Covid 19?

Wakenya wengi wanangoja kwa hamu leo Jumatatu kujua hatua ambazo serikali itachukua hususan endapo rais Uhuru Kenyatta  atatangaza kufunguliwa kwa  nchi na kuruhusu usafiri au kuzidisha mikakati ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Kuna mgawanyiko ulioibuka wa maoni kuhusu kinachofaa kufanywa huku pande mbili zenye maoni tofauti zikijitokeza kutaka  usafairi uruhusiwe na wa pili ukitaka mikakati hiyo ikazwe kamba zaidi kwani visa vya maambukizi ya virusi vya corona vingali vinaongezeka.

Katiba hotuba yake ya mwisho kuhusu hali ya corona rais Kenyatta alisema kurejelewa kwa hali ya kawaida kutategemea iwapo visa vya ugonjwa huo vitakuwa vimepungua na tangazo lake la kuzidisha kipindi cha kafyu liliwashangaza wengi waliomtaraji kuondoa kabisa  kafyu.

Wakati huu, wengi wanapongoja tangazo lake wamejitayarisha kiakili uwezekano wake kuongeza muda huo  ikizingatiwa kwamba  visa vya walio na ugonjwa huo vimeongezeka na sasa wakenya  7,889 wana ugonjwa huo huku 160 wakiaga dunia hadi kufikia sasa.  Siku ya jumamosi Kenya ilisajili visa vingi zaidi kuwahi kuripotiwa kwa siku moja baada ya watu 389 kupatikana na ugonjwa huo hatua ambayo huenda ikafanya kuwa vigumu kwa rais Kenyatta kuamua kulegeza kamba kuhusu masharti  ya kupambana na virusi vya corona.

Je, ni hatua gani zilizochukuliwa na mataifa mengine wakati huu?

 Tanzania

Katika taifa jirani la Tanzania, shule zimefunguliwa ingawaje kuna masharti ya watu kuvalia maski na kuosha mikono katika sehemu za umma. Kenya awali ilikuwa imetanagza kuwa shule zitafunguliwa mwezi Septemba lakini hilo halitawezekana baada ya wizara ya elimu kuzidisha muda huo hadi Januari mwakani. Waziri wa elimu George Magoha amesema walimu, watu takriban laki tatu watapimwa kwanza kabla ya shule kufunguliwa. Hilo huenda likawa jambo gumu kutimiza ikizingatiwa kwamba kwa miezi minne, Kenya imefaulu tu kuwapima watu  189,263.

England

Polisi nchini Uingereza sasa wamesema wamegundua kwamba watu walevi hawana uwezo wa  kujizuia kukaribiana katika usiku ambao maeneo ya burudani yalifunguliwa nchini humo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi mitatu.

Sekta ya utalii na burudani nchini humo imejipata na uchangamfu baada ya   utulivu wa miezi mitatu   na kufunguliwa  siku ya Jumamosi kumewafanya watu kuitaja kama ‘siku ya Uhuru ‘ au super Saturday’

Australia

Australia imetangaza siku ya Jumatatu kwa mara ya kwanza katika miaka 100  kufunga mpaka wa majimbo ya  Victoria na New South Wales. Mara ya mwisho kwa mpaka huo kufungwa ilikuwa 1919 ili kukabiliana na  janga la  Spanish flu

Hatua hiyo hata hivyo huenda ikavuruga uchumi wa  Australia   huku visa vya maambukizi vikipanda katika  mji mkuu wa Victoria  Melbourne  na kuifanya serikali kuanza kutekeleza masharti ya watu kutokaribiana na  hata maagizo ya kutotoka nje yakitolewa .