Raia wa Amerika aliyenaswa akiwatusi wakenya atimuliwa nchini

93bRHkHI.jfif
93bRHkHI.jfif
Jamaa mmoja Mmarekani ambaye alinaswa kwenye video iliyosambaa akiwarushia Wakenya cheche za matusi kupitia simu amefurushwa.

Huku akiwaomba Wakenya msamaha, Balozi wa Marekani nchini Kenya, Kyle McCarter alisema hulka za mwanamume huyo sio za kukubaliwa na ameondoka nchini kufuatia kisa hicho.

"Mwanamume huyo ameondoka nchini. Tabia zake sio za kukubalika. Sina cha kusema zaidi ila  Pole," alisema McCarter kupitia ujumbe kwenye Twitter.

Katika video hiyo, raia huyo wa kigeni anasikika akiwarushia kundi la wakenya cheche za maneno ambao wamesimama nje ya lango la jumba moja jijini Nairobi.

Jamaa huyo ambaye hakutambulika anaonekena akipiga simu ndani ya boma hilo huku umati ukiwa umesimama nje ya lango ukijaribu kuingia kwa lazima ndani ya makazi hayo.

Mmarekani huyo anadai kuwa maisha yake yamo hatarini na kukashifu umati huo kwa kumlaumu kuhusu kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd, ambaye alifariki mikononi mwa polisi, Minneapolis mnamo Mei.

“Niondoe hapa, ninauawa na kundi la watu, wananilaumu kwa kifo cha George Floyd, wote wananilaumu kwa kifo cha George Floyd,” alisema jamaa huyo.

Kulingana na ripoti, mwanamume huyo alinaswa akiendesha biashara haramu kabla ya polisi kuitwa kudhibiti hali hiyo.

Kisa hicho si cha kwanza, huku itakumbuwa mnamo mwaka 2018, raia mwingine wa kigeni alifurushwa baada kumfananisha Rais Uhuru Kenyatta na nyani.

Mchina huyo alifurishwa kufuatia ghadhabu kutoka kwa umma baada ya video hiyo kusambaa mtandaoni.