Rais Kenyatta aonya dhidi ya kukwepa kulipa ushuru

Rais Uhuru Kenyatta ametoa onyo kali dhidi ya kukwepa kulipa ushuru akisema serikali haitasita kuwaadhibu wanaokwepa kulipa ushuru.

Rais alisema serikali haitaruhusu watu wachache kuendelea kulipa kiwango cha chini cha ushuru ikilinganishwa na kile wanachostahili kulipa.

Alisistiza kwamba serikali inabanwa katika utoaji huduma kwa wote huku baadhi ya raia wake wakikosa kutimiza majukumu yao ya ushuru.

“Kwa muda mrefu, hatua ya kukwepa kulipa ushuru imekuwa ya kawaida nchini Kenya. Wakenya wengi wanahisi ni haki yao kudanganya Halmashauri ya Ukusanji Ushuru Nchini KRA, kwa kulipa kiwango kidogo kwa hazina ya kitaifa kinyume na inavyowapasa.

“Lakini, licha ya tabia hiyo, bado wanatarajia kujengwa barabara za kimataifa, kutolewa kwa huduma bora za afya na elimu pamoja na huduma nyingine za umma; huku wakishindwa kutambua  ukweli kwamba bidhaa na huduma hizo zinalipiwa kutokana na ushuru unaokusanywa,” kasema Rais.

Rais Kenyatta alisema haya leo katika hoteli moja Jijini Nairobi alipoongoza dhifa ya mwaka wa 16 ya chakula cha mchana kwa walipa ushuru ambayo iliandaliwa na Halmashauri ya Ukusanji Ushuru Nchini, KRA.

Kwenye sherehe hiyo, ambayo pia ilihudhuriwa na Naibu Rais William Ruto, mashirika mbalimbali yalituzwa kwa kuwajibikia ulipaji ushuru.

Kampuni ya Safaricom ilishinda tuzo la juu kwenye kitengo cha walipaji ushuru wakubwa ilhali kampuni ya Premier Kenya na Paramount Chief ziliongoza katika kitengo cha walipaji ushuru wa kadri na wale wadogo wadogo mtawalia.

Rais alisema ukwepaji kulipa ushuru utakabiliwa vilivyo na akaamrisha mashirika husika ya serikali kutekeleza sheria katika kuhakikisha wale ambao wanadanganya wanachukuliwa hatua kwa uhalifu wao.

“Katika visa vyote, hususan pale ambapo kuna ukwepaji kulipa ushuru au vitendo vingine vya kiuhalifu, sheria sharti ifuate mkondo wake,” kasema Rais.

Alipongeza halmashauri ya KRA kutokana juhudi zinazoendelea za kuwasaka wale wanaokwepa kulipa ushuru akisema maafisa wa usalama wataendelea kuwatia nguvuni na kuwashitaki maafisa wa halmashauri hiyo kwa kusaidia katika vitendo vya uhalifu.

“Ukwepaji kulipa ushuru utapigwa vita kutoka kila upande. Natoa wito kwa walipa ushuru wote kujitokeza kwa hiari na kuwianisha ulipaji wao wa ushuru badala ya kungoja kukabiliwa na dhoruba ya hatua kali zitakazochukuliwa,” kasema Rais.

Rais, ambaye alilipatia jopo hilo miezi mitatu kusuluhisha mizozo yote iliyosalia, alitoa changamoto kwa mahakama kuharakisha uamuzi wa mizozo ya ushuru iliyowasilishwa mahakamani.

“Walipa ushuru na maafisa wa halmashauri ya ushuru wanahitaji kesi zao kusikizwa haraka ili kuwajulisha matokeo yake, katika muda mfupi iwezekanavyo,” kasema Rais.

Alilishauri shirika la KRA kutafuta matumizi ya mbinu mbadala za kusuluhisha mizozo ili kumaliza haraka mizozo hiyo nje ya taratibu ndefu zinazohusika katika mahakama.

“Hakuna haja kumdhulumu mtu aliyetenda makosa madogo. Mtu anaweza kuwa alifanya makosa lakini mnafaa kuketi mkubaliane. Msiitumie halmashauri ya KRA kuwa silaha ya kufanya watu wahalifu,” Rais aliwaambia maafisa wa KRA wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi yake Francis Muthaura na Kamishna Mkuu James Githii Mburu.

Ili kuimarisha mfumo wa ulipaji ushuru nchini, Rais aliamuru Hazina ya Kitaifa, KRA na Mkuu wa Sheria kuanzisha ukaguzi mpya wa sheria za ushuru ili kubuni mfumo thabiti wa kisheria utakaosaidia ukusanyaji na usimamizi bora wa mapato ya kitaifa.

Kama sehemu ya mageuzi, Rais aliagiza asasi hizo tatu kutayarisha mswada na kuuwasilisha katika Baraza la Mawaziri katika muda wa miezi mitatu ijayo.

“Aidha, sharti halmashauri ya KRA iwezeshwe kuleta uwajibikaji zaidi kupitia faini na uwajibikaji katika ushuru kati ya wataalamu wa ushauri na mawakala wa ushuru wanaosaidia kukwepa ulipaji ushuru,” Rais alipendekeza.

Rais Kenyatta aliwatahadharisha wasimamizi wa taasisi wanaokataa kuwasilisha ushuru unaokatwa kutoka kwa mishahara ya wafanyikazi akisema serikali itaanza kuwaadhibu wasimamizi wa mashirika hayo ya serikali wanaokaidi sheria hiyo.

“Hebu fikiria mtu amefanya kazi mwezi mzima na amekatwa ushuru halafu mkubwa wake anakataa kuwasilisha fedha hizo kwa halmashauri inayofaa. Hapo umeibia watu wawili, serikali na afisa huyo mdogo,” kasema Rais akiwahakikishia wananchi kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya maafisa kama hao.

Naibu wa Rais Ruto alisema uhuru wa nchi yoyote unategemea uwezo wa raia wake kulipa ushuru ili kugharamia mahitaji ya kimaendeleo.

Mwenyekiti wa halmshauri ya KRA Balozi Francis Muthaura na Kamishna Mkuu wa KRA James Githii Mburu pia walizungumza katika hafla hiyo.