RambiRambi: Uhuru amuomboleza bintiye Nelson Mandela, Zindzi

Rais Uhuru Kenyatta   ametuma risala za rambirambi  kwa rais wa Afrika kusini  Cyril Ramaphosa,  familia na wananchi wa Afrika Kusini kufuatia kifo cha balozi  Zindziswa Mandela.

Marehemu Zindziswa alikuwa bintiye rais wa zamani wa Afrika kusini Nelson Mandela na mkewe wa zamani   Winnie Madikizela.

Kulingana na  shirika la habari nchini  humo la SABC Zindisziswa  mwenye umri wa miaka 59 anayefahamika pia kwa jina  Zindzi,  aliaga dunia  siku ya Jumatatu na kifo chake kutangazwa na wakfu wa baba yake, Nelson Mandela Foundation.

Zindzi aliaga dunia katika hospitali moja ya   Johannesburg na sababu ya kifo chake haijatolewa.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, rais Uhuru aliitikia familia hiyo ustahimilivu na faraja kutoka kwa Mola wanapoomboleza kifo cha mpendwa wao.

Mandela kabla ya kifo chake alikuwa balozi wa taifa lake nchini Denmark.

Gavana wa Nairobi Mike Sonko katika risala zake alimtaja  Zindzi  kama mwanasiasa aliyekuwa mpole na mcha mungu

Zindzi, alikuwa dadake mdogo  Zenani Mandela  na  alizaliwa  Desemba tarehe 23 mwaka wa 1960  katika eneo la Soweto. Amewaacha watoto wanne, Zoleka, Zondwa, Bambatha  na  Zwelabo.