Ruto amtumia Kalonzo ujumbe kuunda muungano wa kisiasa

RULONZO
RULONZO
Huenda muungano mpya wa kisiasa ukabuniwa kuleta pamoja Naibu rais William Ruto na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Naibu rais amekuwa akitumia wandani wake katika maeneo ya Rift Valley na maeneo ya kati mwa nchi kumfikia Kalonzo. Hatua muhimu tayari zimepigwa.

Gazeti la The Star limebaini kuwepo kwa mazungumzo ya faraghani yalioanza miezi mitatu iliyopita na kufikia sasa mikutano mitatu tayari imefanyika kati ya wandani wa Kalonzo na Ruto kupanga mikakati ya kuunganisha wawili hao.

Wanasiasa hawa wawili wameonekana kutengwa na miungano yao ya kisiasa huku uchaguzi mkuu wa 2022 ukijongea. Duru zaarifu kuwa maafisa wa kiufundi wa Ruto na Kalonzo wanaandaa kanuni za ushirikiano ili kukabili umaarufu wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Raila bado hajatangaza kama atawania urais mwaka 2022 lakini mienendo yake siku za hivi majuzi imeibua maswali mengi kuhusu mipango ya kisiasa ya Raila.

Hofu ya kusambaratika kwa muungano wa Nasa, uliokuwa muungano wa kisiasa wa Kalonzo mwaka 2017 pamoja na mchakato wa uchaguzi mdogo wa Kibra huenda vimechochea mazungumzo baina ya Kalonzo na Ruto kwa lengo la kupanga mikakati ya kunyakuwa urais katika uchaguzi wa mwaka 2022.

Ruto anasemekana kuwatuma washauri wake wa kisiasa kutoka eneo la kati na Rift Valley kuongoza mazungumzo hayo. Mkutano wa kwanza ulifanyika majuma machache baada ya Kalonzo kutuliwa mjumbe maalum wa Sudan Kusini mwezi Julai.

Haijulikani ikiwa Ruto alichangia uteuzi wa Kalonzo ili aunge mkono azma yake ya urais mwaka 2022. Afisa wa cheo cha juu katika chama cha Wiper aliambia The Star kwamba kilichosalia sio kama wataungana bali ni lini ushirikiano wa Ruto na Kalonzo utatangazwa kwa umma.