Ruto sasa amlenga Tuju katiba makabiliano mapya - Jubilee

Naibu rais William Ruto ameazisha makabiliano mapya na mmoja wa marafiki wa karibu wa rais Uhuru Kenyatta, anayeaminika kuwa kizingiti kikuu katika azimio lake kutwaa uongozi wa chama cha Jubilee.

Katika tweet ya kukejeli siku ya Jumapili, Ruto alianzisha mashambulizi makali dhidi ya katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, na kuweka peupe uzito wa tofauti katika chama hicho tawala, huku wengi wakihisi kuwa jahazi la chama hicho linakaribia kuzama.

Lakini wandani wa Uhuru na wale wa karibu na kinara wa upinzani Raila Odinga wanadai kuwa mashambulizi ya Naibu Rais wanamlenga rais Uhuru mwenyewe na Tuju anatumiwa tu kama kisingizio katika siasa za kutafuta uongozi.

Ruto alimshtumu Tuju kwa kuwa miongoni mwa wanasiasa wanao ongoza mipango ya Raila- jamaa anayemuona kama mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa mwaka 2022.

“Kumbe demokrasia ni huria kiasi kwamba katibu mkuu wa chama tawala sasa ni mshauri mkuu wa upinzani!! Maajabu,” Ruto alisema kwenye tweeter.

Lakini ujumbe huo ulizua majibizano makali huku baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wakimwambia Ruto kwamba hata yeye alinufaika kutokana na demekrasia huru, mara nyingi ameenda kinyume na maagizo ya mkubwa wake bila kufutwa kazi.

Tuju ambaye ni mwanafunzi wa siasa wa rais mustaafu Mwai Kibaki, alikataa kujibizana na Ruto, na kuambia gazeti la the Star kwamba ataendelea kuangazia mipango ya rais Uhuru Kenyatta” Huo ndio msimano wangu, kama tu pia ni jukumu langu kujitolea kumuunga mkono rais Kenyatta katika kuafikia mikakati ya kuunganisha taifa kupitia mipango kama ile ya BBI, ushirikiano na upunzani, vita dhidi ya ufisadi na agenda kuu nne,” alisema.

Katika itifaki, Ruto ni mkubwa lakini Tuju ndiye anayesimamia mipango na shughuli za chama cha Jubilee.

Chama hicho hakijaandaa mkutano wowote tangu Uhuru alipoapishwa rais mwaka 2017, na tuju ndiye anaye simamamia mamailioni ya pesa zinatolewa kwa chama hicho kutoka kwa serikali na malipo ya wanachama.

Duru zalisema kwamba malumbano haya mapya yanalenga udhibiti wa chama hicho tayari kwa uchaguzi wa mwaka 2022.