Saratani! Uhuru aahidi kuimarisha sera za kukabili saratani.

Serikali ya Kenya itaimarisha mikakati inayolenga kukabili ongezeko la vifo vinavyotokana na maradhi ya saratani humu nchini.

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Alhamisi aliambia mkutano wa Baraza la Mawaziri katika Ikulu ya Nairobi kuwa Serikali ikishirikiana na washirika wake inachukua hatua ikiwemo kubuni sera ambazo zitasaidia kupunguza athari za ugonjwa wa saratani miongoni mwa Wakenya.

Habari zaidi:

“Tunastahili kuona ni nini tunachoweza kufanya zaidi katika juhudi za kuzuia na pia kutoa tiba ya maradhi hayo. Tunastahili kufanya hilo kama Serikali ya kitaifa kwa pamoja na Serikali za Kaunti,” kasema Rais Kenyatta.

“Hili ni swala ambalo tunastahili kulitilia maanani zaidi na tushirikiane sote kutatufuta suluhisho ikiwemo kinga- ambayo ni muhimu zaidi – lakini pia kuwasaidia Wakenya wenzetu ambao tayari wameathirika na ugonjwa huo kupata matibabu kwa wakati unaofaa,” kaongeza kusema Kiongozi wa Taifa.

Habari zaidi:

Rais Kenyatta ambaye aliongoza baraza la mawaziri katika kutoa heshima kwa marehemu Gavana wa Kaunti ya Bomet Dkt. Joyce Laboso na mbunge wa Kibra marehemu Ken Okoth kwa kukaa kimya kwa dakika moja, wote ambao walifariki juzi kutokana na maradhi ya saratani, alisema kwamba saratani ni ugonjwa unaoendelea kuwa tatizo kubwa ambalo linalohitaji kushughulikiwa kwa haraka.