Serikali yaanzisha kampuni ya kutoa mikopo ya Nyumba

Rais Uhuru  Kenyatta leo amezindua kampuni  ya kutoa mikopo ya ujenzi wa Nyumba (Kenya Mortgage Refinance Company ) ili kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wanaotaka kufadhili ujenzi wa nyumba.

Kampuni hiyo  inayaleta pamoja mashirika mbali mbali ya kifedha ambayo yameweka raslimali pamoja ili kuweza kutoa mikopo kwa wakenya .Mikopo ya ujenzi wa nyumba imekuwa ya gharama ya juu sana kwa wakenya wengi na serikali inatumai kwamba kampuni hiyo mpya itaweza kuziba pengo hilo na kumaliza uhaba wa nyumba unaoshudia  kwa sasa nchini .

KMRC,  itaanza oparesheni zake ikiwa na mtaji wa mwanzo wa shilingi bilioni 35  na ilianzishwa kama taasisi ya kifedha isiochukua akiba  chini ya uangalizi wa benki kuu ya Kenya .

Mkopo wa kwanza kuipiga jeki kampuni hiyo ulitoka kwa benki ya Dunia iliyotoa shilingi bilioni 25  na Benki ya Maendeleo barani afrika  iliyotoa shilingi Bilioni 10. Rais  Kenyatta amesema mpango huo wa KMRC ni ushirikiano kati ya serikali na  Sekta ya kibinafsi .