Siku arobaini zatimia: Wanawake 4 wamulikwa na CCTV wakiiba mali dukani

d0ed3521b90b7c78
d0ed3521b90b7c78
Arobaini za wanawake wanne zilitimia baada ya kunaswa kwa kuhusika katika wizi wa bidhaa katika maduka ya jumla kaunti ya Busia. Polisi walisema wanne hao ni miongoni mwa genge sugu la wahalifu ambao wamekuwa wakipora bidhaa katika maeneo ya Magharibi na Nyanza.

Washukiwa walinaswa Jumatano, Juni 19 ndani ya duka la Peshmart wakiwa wameficha bidhaa za kuibwa katikati ya miguu yao.

Hii ni mara ya pili washukiwa hao wananaswa baada ya kukamatwa Jumapili mjini Kisumu wakitekeleza uhalifu huo dukani. Picha za kamera za usalama, CCTV zilionyesha kwamba siku iyo hiyo walipora mali katika maduka ya Frankmart na Khetias ya maeneo ya Busia kabla ya kukamatwa Bumala.

Haya yanajiri baada ya wasimamizi wa maduka yaliyoathirika kulalamika kuhusu hasara waliyokadiria kutokana na kutoweka kwa bidhaa.

Kulingana na kamanda wa eneo bunge la Butula Richard Omanga washukiwa hao wanatokea kaunti ya Vihiga. Washukiwa hao ambao walinaswa na gari linaloaminika kutumika katika usafirishaji wa mali hiyo wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Bumala huku uchunguzi zaidi ukiendelea.