Caroline Flack
Wa kwanza ambaye hakustahili uvamizi uliolenga maisha yake binafsi ni Brenda Cherotich ambaye serikali ilitangaza kwamba alikuwa amepona virusi vya Corona. Licha ya baadhi ya wanamitandao kutoamini masimulizi yake kuhusu safari yake nzima ya kuambukizwa ugonjwa huo na baadaye kutengwa katika karantini wakati akipona , wengi walianza kuzisambaza picha zake za zamani katika jitihada za kumdhalilisha .
Kilichowavunja wengi nyoyo ni kuanza kusambazwa kwa picha za utupu za Brenda katika hatua ya kujaribu kumfanya ajihisi mtu duni . Baada ya hilo, mtangzaji wa Runinga Yvonne Okwara alipojaribu kukosoa tabia hiyo naye pia akawekwa chini ya kaa la moto kwa mashambulizi yaliolenga maisha yake bila kujali kwamba alikuwa na haki ya kutoa maoni yake .
Kinachochochea umuhimu wa dharura wa kuchukua hatua za kuzuia uenezaji wa chukio mitandaoni ni kisa cha mapema mwaka huu ambapo mtangazji wa runinga kutoka Uingereza Caroline Flack alijiua katika hali ya kutatanisha baada ya kuelekezewa chuki chungu nzima katika mitandao ya kijamii . Flack alikuwa mtangazaji wa kipindi cha ‘Love Island’ na kifo chake kiliutukiza ulimwengu na hasa waliokuwa wakifuatilia vipindi alivyokuwa akishirikishwa. Wengi walishangaa ilikuwaje kwa mtu mashuhuri kama yeye kufika mwisho hadi akaamua kujiua lakini sasa rafiki zake wa karibu wameanza kutoa ufichuzi wa jinsi Flack alivyosumbuliwa fikra na mashambulizi kutoka kwa watumiaji wa mitandao .