Siri imetoboka! Jinsi wakazi wa Nairobi hujipata kwenye ndoa

Ukifuatilia kwa makini, mahusiano na pia ndoa nyingi humu nchini, haswa mjini Nairobi yalianzia kwa njia za ajabu na zingine za kuchekesha sana. Na hatuangazii mahusiano ya vijana wa kizazi cha lakini pia itabidi tulinganishe jinsi wapenzi wa enzi za wazazi wetu walivyokuwa wakichumbiana na pia jinsi walivyojipata kwenye ndoa.

Kwa mfano, enzi za kale wawili wangepatana kwa njia tofauti, aidha sokoni, shuleni na hata pia kwa njia tu ya kuwa majirani. Hapo wewe kama kijana au msichana utatafuta mbinu ya kujitambulisha na kufanya nia yako ieleweke kwa kuwa karibu na umtakaye.
Hapo kama mioyo yenyu itaelewana na muamue kuchumbiana mara nyingi mahusiano yaliishia kuwa ndoa.
Siku hizi hata haupaswi kuishi karibu na vidosho ila ukitaka kutafuta mpenzi kuna njia nyingi mno za kuwapata. Njia moja ni kupitia kupatana katika gari za abiria, waweza patana nao katika maeneo ya burudani na rahisi mno ni kupitia mitandao ya kijamii ambapo kwa kuwacha tu ujumbe kwa picha ya unayemezea mate kwaweza kupelekea mambo mengi.

Usisahau kuwa kuna wanandoa wengi ambao wamekiri kupatana kupitia mitandao ya kijamii. Kando na hayo yote waweza pata watu ambao nia yao sio 'kujibamba' tu nawe au kuwa tu na uhusiano wa miezi michache ila kinyume na wapenzi wao, wataka uhusiano utakao dumu milele, al maarufu ndoa.
Leo nataka tuangazie njia kadhaa tata na za kushangaza ambazo wana Nairobi hutumia na ambazo pindi tu umefumba na kufumbua, unajipata kwenye uhusiano au ndoa hukuwa umetarajia.
Mimba
Hili utakubaliana nami kuwa wanadada wengi wamekuwa wakitumia njia hii kuwateka wanaume na kulazimisha wengi kuingia kwenye ndoa hawakuwa wametarajia. Unajipata kwenye uhusiano wa kimapenzi, na baada ya kuonana kimwili mara kwa mara siku moja mwanadada anakupasulia mbarika kuwa michezo yenyu itawazalia matunda.

Hapo na hapo hata kama hukuwa na mipango ya kumuoa yule mwanadada inakulazimu kumuoa au kuingia kwenye uhusiano naye.
 
'Kutekana'
Nimetumia jina kutekana kwa mabano kwani nimetafuta jinsi ya kutafsiri jina 'One night stand' ambalo mara kwa mara lajulikana kama kutekwa ama kutekana. Sanasana hili hutokea pale ambapo uko klabuni na unapatana na mwanadada anayekuchizisha au yeye anapatana na kijana mtanashati. Katika hali ya kujuana na kujibamba mnaamua kwenda nyumbani pamoja.
Usisahau lengo lenyu wawili halikuwa uhusiano bali mlivutiana tu na mkaamua kushiriki mapenzi. Basi baada ya siku ile mnaamua kupatana tena mara kwa mara, na katika ile hali ile hali ya kuvutiana inazaa jambo kuu na kabla mjue, mnajipata katika uhusiano.
Rafiki wa chanda na pete
Kumekuwa na mijadala mikali kwa mda sasa kuhusu swala la kuwa na rafiki wa chanda na pete yaani best friend wa jinsia tofauti na yako.
Hii ni kwa sababu wengi husema kuwa hakuna vile mtakuwa tu na urafiki mtupu bila nyinyi kujipata katika hali ya kutongozana au kushiriki mapenzi kwani mko pamoja karibu kila mara.
Kuna wapenzi ambao watakufungukia kuwa kuna muda walikuwa tu marafiki wa chanda na pete na hawakuwa na hisia za kimapenzi. Lakini jambo moja au mawili yakatokea na wakajipata wakitongozana na sasa wamefunga ndoa.
Wengine walikuwa katika hali ya kuwapa marafiki zao bega la kulilia pindi walipotengana na wapenzi wao na katika hali ile hisia zikawazidia na hivi sasa ni mabibi na mabwana.

Tuokoe kodi

Kabla ukunje uso wako niskize kwanza.
Haya sote twajua mahusiano kwenye maeneo ya kazi ni jambo ambalo unapaswa kujiepusha nalo lakini haimaanisha sio halali. Basi hili linamaanisha kuna wafanyikazi ambao wana uhusiano labda wenzao wanajua na labda wengine wanachumbiana kisiri.
WIki au miezi michache baada ya kutongozana, hapo ndipo utapata mmoja wenyu ameanza kupendekeza kuwa haina maana nyinyi wawili kuwa na nyumba mbili tofauti na mnaenda mahala pamoja kila asubuhi.
Hapo anapendekeza kuwa muishi pamoja jambo ambalo pia litawasaidia kuokoa kodi fedha ambazo mwaweza tumia kwa matumizi mengine. Ghafla bin vuu unajipata kwenye ndoa hukuwa umepangia.