Sote tuna wajibu wa kukabiliana na ufisadi, asema Rais Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta amewahimiza Wakenya washirikiane katika kushughulikia changamoto zinazokumba nchi hii.

Rais alisema kila Mkenya ana wajibu wa kukabiliana na ufisadi na maovu mengine yote ambayo yanazuia ustawi wa nchi.

“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha tunakabiliana na ufisadi, tunalinda mazingira na tunashirikiana kuhakikisha kuna amani.

“Iwapo kila mmoja wetu atatimiza jukumu lake ipasavyo, sioni sababu ya kwa nini hatuwezi kukabiliana na changamoto zinazotukumba,” kasema Rais.

Rais Kenyatta alisema haya leo katika madhabahu ya Marian yalioko Subukia, kaunti ya Nakuru ambako alijiunga na  waumini wa Kikatoliki kwa uzinduzi wa kampeini ya kitaifa ya kwaresima ya mwaka huu na kutolewa kwa waraka wa wachungaji.

Kiongozi wa Taifa  alisema haina haja ya kulaumiana na kusingiziana wakati mambo yanaharibika akisema badala yake wananchi wapaswa kujichunguza na kutafuta suluhisho ndani mwao.

“Iwapo tutarekebisha njia zetu na kuzingatia jinsi ya kutatua matatizo badala ya kutoa lawama basi tutafaulu katika kujenga taifa hili tukufu,” kasema Rais.

Kuhusu harakati za Uwiano yaani BBI, Rais Kenyatta alisema Wakenya wana fursa ya kuwasilisha maoni yao na kuhakikisha kwamba mashindano ya kisiasa kamwe hayatasababisha umwagikaji wa damu, vifo na uharibifu wa mali nchini.

Alisema harakati za uwiano zitahakikisha watu wanashindana kisiasa katika misingi ya sera na wala sio katika misingi ya kikabila ambayo kila mara imesababisha maafa.

“Ukabila hautaboresha maisha yako lakini maono na sera nzuri zitafanya hivyo. Na maono hayo yanaweza kutoka kwa Mkenya yoyote kutoka sehemu yoyote ya nchi.

“Iwapo tutaongozwa  kwa sera nzuri, sina shaka kutakuwa na amani na Wakenya hawataishi kwa hofu inayoshuhudiwa kila wakati wa uchaguzi,” kasema Rais huku akiwahimiza waumini wa katoliki kueneza injili ya amani na ya kukabiliana na ufisadi wakati huu wa msimu wa kwaresima.

Ibada hiyo maalumu iliongozwa na  Mwenyekiti wa Muungano wa Maaskofu wa Katoliki nchini Most Rev Philip Anyolo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kisumu huku mahubiri yakitolewa na Askofu mkuu Martin Kivuva.

Maudhui ya kampeini ya Kwaresima ya mwaka huu ni “Utumishi kwa Taifa la Mabadiliko… Wajibu wangu,” ambayo inawiana na kampeini ya kukabiliana na ufisadi iliyozinduliwa na Muungano wa Maaskofu wa Kikatoliki mnamo mwezi Oktoba mwaka jana.

Askofu Anyolo aliwahimiza Wakenya  kusimama pamoja  na kuvunja nyororo za ufisadi.

“Tumejitolea kukabiliana na ufisadi na tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe neema ya ujasiri kushinda changamoto hii,” kasema Askofu Anyolo.

Katika desturi ya Kikatoliki, Kwaresima ni kipindi  cha kuanzia Siku ya Jumatano ya Ibada ya majivu hadi Jumapili ya Mtende na ni ibada inayoadhimishwa  kila mwaka kwa kuwatayarisha waumini kupitia maombi, toba, kutoa sadaka na kujinyima.